Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (Mewata) kimefanya kongamano kubwa la kisayansi la kujadili changamano za masuala ya afya hususani saratani ya kizazi na magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Kongamano hilo ambalo limekutanisha madaktari, wanasayansi na wadau mbalimbali wa masuala ya afya lilifanyika Dar es Salaam jana katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kufunguliwa na Waziri wa Afya za Zanzibar, Nassoro Ahmed Mazrui.
Kongamano hilo litafuatiwa na Mkutano Mkuu wa 20 wa Mewata utakaofanyika kesho katika ukumbi huo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 35 tangu kuanzishwa kwa chama hicho kisicho cha kiserikali, ambacho malengo yake makuu ni kusaidia, kuhamasisha na kutoa elimu mbali mbali zinahusiana na magonjwa na afya ya mama na mtoto.
Akizungumza wakati wa kongamano hilo, Rais wa Mewata,Zaituni Bokhary alísema Mewata imejikita katika kupambana na magonjwa ya saratani yanayoshambulia wanawake kwa asilimia kubwa, hususan saratani ya mlango wa kizazi, na saratani ya matiti.
Alisema pia kinahamasisha watoto wakike kujiunga na fani za udaktari ili baadae wawe madaktari kwani huko nyuma, fani ya udaktari ilikuwa ni kwa ajili ya wanaume tu, hatua ambayo imeleta mafanikio makubwa kwani sasa kuna idadi ya kutosha ya madaktari wanawake na inaendelea kukua.
Bokhary alisema chama hicho kimefanya mazoezi ya kupima afya za kina mama katika mikoa mbalimbali nchini ikiwamo, Dar es Salaam, Mbeya, Lindi, Mtwara, Kilimanjaro, Njombe, Iringa, Tabora, Dodoma, Songea na Mwanza.
“Katika mazoezi haya, tulifanikiwa kuwafanyia uchunguzi wa awali wa saratani ya matiti wakina mama takriban 73,744, na uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi kina mama 9,307. Tuligundua kina mama wengi wana matatizo mengi ya kiafya hususan magonjwa ya saratani na uelewa mdogo wa maradhi haya.
Hii ilipelekea wamama wengi kuripoti hospitali wakiwa wamechelewa au wako katika hatua za mwisho za ugonjwa na kuchangia vifo vingi vitokanavyo na saratani kwa kina mama’ alisema.
Aisha, alisema pamoja na hilo, Mewata kwa kushirikiana na serikali imefanikiwa kuhamasisha wanafunzi wa kike wa sekondari kuchukua masomo ya sayansi na kuongeza idadi ya madaktari wanawake Tanzania na pia kimeweza kuwajengea uwezo madaktari na kupelekea kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali katika serikali na taasisi binafsi.
Katika hatua nyingine, profesa Mwaikambo alisema Mewata ina mpango wa kujenga hospitali katika eneo la Mbweni, Dar es Salaam kwa msaada wa serikali ya Japan kupitia mama mlezi wa chama, mama Salma Kikwete.
“Kwa sasa tumehamasishana wanachama na tumeweza kukusanya kiasi cha shilingi milioni 31,530,000 za kitanzania fedha taslim na milioni 46,530,000 zikiwa ni ahadi” alisema.Rais huyo wa mewata alisema chama hecho kinatambua mchango mkubwa unaofanywa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kupambana na vifo vinavyotokea vya mama na mtoto, hivyo madaktari wanawake wanaunga mkono juhudi zinazofanywa na Raisi Dk Samia Suluhu
Hassan.
“Tunatambua Mheshimiwa Rais anapambanakatika kuhakikisha hakuna mama anayekufa kwa sababu ya uzazi, hivyo amepeleka huduma muhimu karibu kabisa na makazi ya watu.Aidha, Mewata inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Mh Rais Dkt Hussein
Ali Mwinyi katika kuboresha huduma za afya Visiwani Zanzibar kama kujenga na kuongeza vituo vya afya na kuboresha maslahi ya
madaktari” alisema.
Waziri WA AFYA Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui akizindua kitabu kuhusu wasifu wa mwasisi WA Chama Cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), Profesa Esther Mwaikambo (kulia) kwenye kongamano la 20 la Kisayansi la chama jicho jijini Dar es Salaam