Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MADIWANI wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, wakuu wa idara na vitengo, wamepewa mafunzo ya maadili ya viongozi wa umma, ambayo ndiyo nguzo kuu katika utendaji kazi na kusukuma gurudumu la maendeleo kwa wananchi wa eneo hilo.
Afisa maadili ya viongozi wa umma kanda ya kaskazini Adam Kuhanda, amesema uzingatiaji wa maadili ni muhimu sana kwa viongozi wa umma na kufanya vizuri katika utendaji wao kazi.
“Maadili ni kinga kwa viongozi na kuna utafiti umefanyika kuwa asilimia 80 ya mafanikio kwa viongozi ni kuzingatia maadili na maadili huwa yanafanya viongozi kuwa waadilifu katika utendaji kazi na kufikia malengo yao,”amesema Kuhanda.
Ametaja faida ya maadili kwa viongozi wa umma, kuwa yatawafanya kutoa maamuzi sahihi, kuwa wawajibikaji na wawazi, kufanya kazi kwa pamoja (Teamwork), kupendana, kuheshimiana na kushauriana namna ya kufanya kazi na kufikia malengo waliyojiwekea.
Katika hatua nyingine ametaja vitendo visivyo vya maadili kwa viongozi wa umma, kuwa ni kutumia madaraka vibaya na kujipatia fedha isivyo halali, kuweka shinikizo ili mtumishi wa umma afukuzwe kazi kinyume cha sheria na kutumia lugha za matusi.
Ameendelea kutaja vitendo vingine visivyo vya maadili kuwa ni kuegamia upande mmoja wakati wa kutatua migogoro, kupingana kauli hadharani na kiongozi mwingine.
“Nyingine ni kupokea zawadi ya fedha ambayo inazidi shilingi 200,000 na kuwa chanzo cha kuanzisha migogoro badala ya kuwa kimbilio la suluhisho,” amesema Kuhanda.
Hata hivyo, Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro, Jacob Kimeso amesema mafunzo hayo ya maadili kwa viongozi wa umma yamewagusa vyema na kuongeza tija katika utumishi wao.
Kimeso amewataka viongozi, madiwani na watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro wayazingatie na kuwaongoza katika utumishi wao wa wananchi wa eneo hilo.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Simanjiro Kiria Ormemei Laizer amesema mafunzo hayo kwa namna moja au nyingine yatawafanya viongozi hao kubadilika na kutimiza wajibu wao ipasavyo.
“Mafunzo kama haya yanapaswa kufanyika mara kwa mara ili viongozi wakumbushwe wajibu wao katika kuwatumikia wananchi kupitia Serikali inayoongozwa na CCM,” amesema Kiria.