Na WAF- SIHA KILIMANJARO.
WANAKIJIJI wa Lekirumuni kata ya Karanzi Wilaya ya Siha Mkoa wa Kilimanjaro wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuwaletea maendeleo ikiwemo ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Siha, ujenzi wa barabara, ujenzi wa shule, na kusambaza huduma za umeme kwa wananchi.
Hayo yamejiri wakati Waziri wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea katika kijiji cha lekilumuni katika Kongamano la mazingira lililokuwa likifanywa na jamii ya kimaasai kutoka maeneo mbalimbali ndani na nje ya nchi.
Wakati akiongea na wanakijiji wa jamii hiyo ya ufugaji (Wamasai), Waziri Jenista amefurahishwa na idadi kubwa ya watu wa jamii hiyo waliojitokeza katika Kongamano hilo la mazingira na kuwapa salamu kutoka kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan la kuwataka kuendelea kuchapa kazi ili kuleta maendeleo.
Ameendelea kusema, “Mkusanyiko huu unatoa sauti ya pamoja ya kumshukuru Chief Hangaya (Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan) kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, nimefarijika sana.”
Aidha, ameweka wazi kuwa, ni dhahiri kusanyiko hilo lililomshukuru Mhe. Rais ni uthibitisho wakutosha kwamba 2025 Dkt. Samia Suluhu Hassan ataendelea kuwa Rais ili kuendeleza kazi nzuri aliyoifanya ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Sambamba na hilo, Waziri Jenista ametoa wito kutumia Kongamano hilo kujadili namna bora ya kuwafunza maadili vijana na watoto ili kutunza mila na desturi zetu licha ya maendeleo ya teknolojia na utandawazi yanayochangia mmong’onyoko mkubwa wa maadili.
Nae, Mbunge wa Jimbo la Siha na Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel amemthibitishia Waziri Jenista kuwa, katika eneo ambalo Rais Samia atapata kura zote 2025 ni jimbo la Siha, hali inayotokana na kazi kubwa ambayo ameifanya ya kuwaletea maendeleo wana Siha ikiwemo ujenzi wa barabara za rami, ujenzi wa shule mpya, usambazaji wa huduma ya umeme na maji pamoja na uboreshaji wa huduma za afya katika hospitari ya Wilaya ya Siha pamoja na Kibong’oto.