Mbunge wa viti maalum mkoani Ruvuma Mariam Nyoka,akizungumza na baadhi ya wakazi wa kijiji cha Wenye katika Halmashauri ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma ambapo pamoja na mambo mengine amewahimiza vijana wa wilaya hiyo kufanya kazi kwa bidii ili kujiletea maendeleo yao badala ya kutumia muda mwingi kukaa vijiweni kusubiri ajira.
Na Muhidin Amri,
Tunduru
VIJANA wa wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,wametakiwa kuacha tabia ya kulalamika badala yake wazitumie fursa za kiuchumi zilizopo kwa wingi katika maeneo yao kubuni miradi na kufanya kazi kwa bidii na kujiletea maendeleo yao ili kuepuka tabia kuomba omba.
Kauli hiyo imetolewa jana na Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka,wakati akizungumza na baadhi ya vijana wa kijiji cha Wenje kata ya Nalas akiwa katika ziara yake ya kukagua na kuhimiza shughuli mbalimbali za serikali wilayani humo.
Alisema,ili mtu aweze kufanikiwa kimaisha haitaji zaidi ya elimu ya darasani bali ni muhusika mwenyewe kujiongeza kufanya kazi kwa kujituma kwa kila jambo ambalo anatamani kulifikiria na kulifanya.
Nyoka alisema,tatizo la vijana wengi katika wilaya ya Tunduru kukabiriwa na changamoto ya ukosefu wa ajira na umaskini linatokana na wengi wao kushindwa kubaini na kuzitumia fursa zilizopo katika maeneo wanayoishi na hivyo kuishia kulalamika na kuilaumu serikali yao.
Alisema,hali hiyo inatokana na jamii kukosa moyo wa uthubutu kuingia katika kazi halali za kuwapatia kipato na kujikuta wakitumia muda mwingi kukaa vijiwemi na kusubiri serikali iwatafutie ajira,jambo ambalo limechangia vijana wengi kuendelea kuwa maskini.
Amewashauri vijana wilayani Tunduru,kuungana ili kupata mikopo isiyo na riba kutoka serikalini na kuwa chanzo cha mapinduzi ya kiuchumi na kuacha kufanya kazi bila malengo na kusisitiza kuwa,vijana wana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi yetu.
Ametoa wito kwa vijana wa kijiji hicho ambacho kinapakana na nchi jirani ya Msumbuji,kuendelea kulinda na kutunza amani iliyopo na kuepuka kutumiwa kuvuruga mashikamano na utulivu uliopo kwa muda mrefu na kutoa taarifa pindi wanapobaini kuwepo mtu wanayemtilia shaka katika maeneo yao.
Katika hatua nyingine Nyoka,amewataka viongozi wa ngazi mbalimbali, kuhamasisha wananchi wao kuitumia miundombinu inayojengwa na serikali katika maeneo mbalimbali zikiwemo barabara kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Ameipongeza serikali ya awamu ya sita kupitia wakala wa barabara za vijijini na mijini Tanzania(Tarura)mkoa wa Ruvuma kwa kazi nzuri inayofanya ya matengenezo ya barabara ambazo zimewezesha kupitika majira yote ya mwaka na kutoa fursa kwa wananchi wa mkoa wa Ruvuma kufanya shughuli za kujiletea maendeleo.