Waziri wa ujenzi na uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa akipata maelezo ya mradi huo kutoka kwa Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi akiwa ziarani mkoani Arusha.
Kaimu Meneja wa TBA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi akitoa maelezo juu ya mradi huo kwa Waziri wa ujenzi na uchukuzi alipotembelea mradi huo jijini Arusha.
Julieth Laizer ,Arusha.
Waziri wa uchukuzi na ujenzi Profesa Makame Mbarawe leo ametembelea mradi wa ujenzi wa wakala wa majengo Tanzania (TBA) Mkoa wa Arusha na kuridhishwa na kasi ya ujenzi huo pamoja na thamani halisi ya fedha zilizotumika kuendana na mradi huo.
Hata hivyo amesema kuwa, mradi huo umefanyika kwa umakini mkubwa na fedha zilizopangwa kutumika katika mradi huo zinaendana na mradi wa jengo hilo.
Akizungumza mara baada kutembelea jengo hilo katika ziara yake mkoani Arusha,Mbarawa amesema jengo hilo linaendana na thamani ya fedha ambazo zinatokana na mapato ya ndani ya taasisi hiyo.
Hata hivyo Waziri amesema kuwa, wamejipanga kuhakikisha wanatumia mfumo maalumu wa kitasa janja(Smart Lock) kwenye nyumba hizo ili kudhibiti uwepo kwa wadaiwa sugu ambao wamekuwa wakisumbua kulipa pango la nyumba.
“Sasa hivi hatutaki kusumbuana tena na wapangaji wetu ambao hawataki kulipa kwa wakati tukitumia mfumo huo maalumu ikifika mwisho wa mwezi tunampa mteja onyo la kulipa kwa muda wa wiki moja tukiona hajalipa tunampa tena onyo la pili kwa muda wa siku tatu baada ya hapo asipolipa mfumo wa smartlock unafanya kazi yake kila akitaka kuingia ndani inagoma hadi alipie bango la nyumba na hiyo ndio njia nzuri ya kuwabana wadaiwa sugu na kuepukana kusumbuana nao hadi mahakamani.’amesema Waziri Mbarawa.
Kwa upande wake Kaimu Meneja TBA mkoa wa Arusha ,Mhandisi Juma Dandi amesema kuwa jengo hilo lina uwezo wa kuchukua familia 22 ambavyo ni kitega uchumi cha TBA ambapo wapangaji katika nyumba hiyo watapaswa kulipa kwa wakati kwani wanapokea hela kila mwezi.
Amesema kuwa mradi wa jengo hilo lenye ghorofa 10 umeshatumia kiasi cha shs 5.2 bilioni hadi sasa ambapo mpaka kukamilika litagharimu Kiasi cha shs 5 .5 bilioni na unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya wiki mbili hadi tatu .
Aidha Mhandisi Juma amesema kuwa,kukamilika kwa mradi huo kutaweza kukidhi mahitaji ya makazi kwa watumishi wa umma na mapato ya serikali kwa ujumla na uwepo wa mradi huo umeweza kuongeza idadi kubwa ya ajira kwa mafundi na wafanyakazi wengine pamoja kuwepo kwa ununuzi mkubwa wa vifaa vya ujenzi .