******************
NJOMBE
Abiria hususani wagonjwa kutoka maeneo tofauti ya Tanzania wanaofata matibabu katika hospitali ya Consolatha Ikonda wilayani Makete mkoani Njombe wamelalamikia kitendo cha serikali kupiga marufuku matumizi ya kituo cha mabasi cha Ikonda na badala yake wakitakiwa kutumia kituo kipya cha Tandala kilichopo umbali wa km 2 kutoka hospitalini hapo kwa madai ya kwamba maruku hiyo imeongeza usumbufu na kuweka hatarini usalama kwa wagonjwa wenye hali mbaya .
Hospitali ya Consolatha Ikonda imekuwa kimbilio la wengi kutoka maeneo tofauti ya Tanzania kutokana na huduma zake ambapo inakadiriwa zaidi ya wagonjwa 300 hufika kupata tiba jambo ambalo lililazimu kujenga kituo kidogo cha mabasi ambacho kimetumika kwa miaka mingi hadi sasa ili kuepusha usumbufu kwa wagonjwa.
Kufuatia katazo hilo lililokuja punde baada ya halmashauri kuanzisha mradi wa kituo kidogo cha Tandala kilichopo mbali na hospitalini ikonda ,Kinawaibua wagonjwa na abiria wengine wanaofata matibabu akiwemo Moris Mgaya kutoa hisia zao ambapo wanasema maisha yao yamekuwa hatarini hasa nyakati za usiku kwasababu wanalazimika kupanda pikipiki na wagonjwa mahututi huku wengine wakikiri kuzurumiwa fedha na bodaboda .
“Tunalazimika kukodi bodaboda ambapo tunalipa elfu mbili na usiku gharama huongezeka huku wengine wanaamua kutembea kwa mguu kwenda hospitali jambo ambalo ni hatari kwa maisha yetu,wengine wagonjwa mahututi wanapanda bodaboda hivyo tunaomba serikali iruhusu stendi ya Ikonda hospitali iendelee kutumika ili kutupunguzia gharama na usumbufu,alisema Agnes Msigwa Mgonjwa”Malalamiko ya wagonjwa yamenilazimu kufunga safari hadi kwa mkurugenzi wa hospitali ya Consolatha Ikonda Padre William Mkalula ambaye anasema katika kipindi cha siku nne wameonja usumbufu mkubwa kwa wagonjwa na kulazimika kutumia magari ya hospitali kufata wagonjwa waliyozidiwa kituo cha Tandala.
Amesema wao hawaathiri na kituo cha kidogo cha mabasi cha Ikonda kufungwa lakini wanapata wakati mgumu wanapoona wagonjwa wanateseka kupanda bodaboda wakati hapo mwanzo walikuwa wanaletwa na mabasi hadi hospitalini.
“Siku chache zimepita tangu tulazimike kutumia gari la hospitali kufata mgonjwa aliyezidiwa pale Tandala na kisha kuja kufanyia upasuaji ambapo hadi sasa yupo ICU,alisema Padre William Mkalula mkurugenzi wa hospitali ya Consolatha Ikonda”
Wakati uamuzi huo wa serikali ukionekana kupingwa vikali na wagonjwa pamoja na baadhi ya abiria na wakati wa kata ya Ikonda ,Diwani wa kata ya Tandala nae Daniel Hatanaka anasema kilichofanyika kinakwenda kuwaumiza wagonjwa hivyo halmashauri inapaswa kuona namna ya kuweka sawa jambo hilo ili vituo vyote viwili vitumike.
Hatanaka anasema haiwezekani mgonjwa alifanyiwa upasuaji ,aliyevunjika mguu ama mgongo kupanda bodaboda hivyo anaomba kituo cha Ikonda kiruhusiwe kushusha abiria hususani wagonjwa kwakuwa katika kituo kipya hakuna usafiri wa uhakika.
Akifafanua sababu ya kupiga marufuku matumizi ya kituo cha mabasi cha Ikonda Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete William Makufwe anasema ni kuiweka mbali stendi na hospitali lakini pamoja na kikwazo hicho serikali imetoa ruhusa kwa baadhi ya mabasi kufika kabisa hospitali endapo yatakuwa yamebeba wagonjwa wenye hali mbaya.
Makufwe amesema suala la kusitisha matumizi ya kituo kidogo cha mabasi cha Ikonda ni maazimio ya baraza la madiwani na watalaamu hivyo wanafanya hivyo kwakuwa serikali imeweka zaidi ya mil 100 katika mradi huo huku pia akisema wanachokitazamia sasa ni kuboresha mazingira na huduma za usafiri.
“Hatuwezi kuruhusu kituo cha mabasi kuwa jirani na hospitali hivyo kwasasa itatumika stendi ya Tandala kama baraza lilivyoazimia na halijaanza leo suala hili,alisema Makufwe mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Makete.
Awali mabasi yalikuwa yakiingia kushusha wagonjwa katika kituo cha mabasi Ikonda na kisha kuendelea na safari kwenda makete mjini na maeneo mengine lakini kwasasa serikali imefungua kituo cha mabasi cha Tandala kilichombo mile kadhaa kutoka Ikonda Hospitali jambo linalosababisha usumbufu kwa wagonjwa.