Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Kamati ya Uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya viongozi hao, katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu, Kusini Unguja, Zanzibar
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson, akizungumza na Kamati ya Uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge, kwenye ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu, Kusini Unguja, Zanzibar
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akisalimiana na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya Kamati ya Uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge katika ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu Kusini Unguja Zanzibar
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Kamati ya Uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za kudumu za Bunge, kwenye ufunguzi wa mafunzo ya viongozi hao, kwenye ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu, Kusini Unguja, Zanzibar Februari 28, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Kamati za Kudumu za Bunge watambue mchango wa Asasi za kiraia katika kazi zao kwa kuwa zina changia maendeleo Taifa.
Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Februari 28, 2023) alipofungua mafunzo ya kamati ya uongozi na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge, kwenye ukumbi wa Ofisi ndogo ya Bunge, Tunguu, Kusini Unguja Zanzibar
“Sote tunafahamu mchango wa asasi za kiraia nazo pia lazima tuzifahamu, tunazo asasi za kiraia ambazo tumeweka mikataba nayo, ni muhimu kulizingatia, uwezo wa Serikali pekee hautoshi, Bunge mtapata fursa ya kukutana nazo kwenye kamati zenu, lazima mtambue mchango wake na uwe na maslahi kwa Taifa”
Amesema kuwa ni muhimu kamati hizo kuhakikisha asasi hizo zinatekeleza majukumu ya kimsingi ambayo wamekubaliana na Serikali kwa maslahi ya jamii yetu na si kubeba ajenda ambazo hazina maslahi kwa jamii yetu.
“Ni muhimu sana viongozi wenzangu mkazingatia yale mambo ambayo yanavunja maadili, miiko, mila na utamaduni wetu, sisi wabunge ukiwa kwenye kamati yako ukiona moja ya asasi inaenda kinyume na yale tuliyokubaliana msiache kuyaleta mezani, malengo ya kamati hii ya uongozi ni kuishauri Serikali kuendesha nchi katika kukuza maslahi yetu kimaendeleo na maadili tuliyonayo”
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa mafunzo hayo yatatoa fursa kwa Wajumbe kukaa pamoja na kukumbushana masuala mbalimbali, kujadili mafanikio na changamoto pamoja na kuweka mikakati ya kiuendeshaji na utendaji wa Kamati za Bunge na Bunge kwa ujumla.
“Ni matumaini yangu kwamba wajumbe na washiriki wa mkutano huu watatumia vizuri fursa hii ya kuwa hapa pamoja kujifunza, kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi, usimamizi na uendeshaji wa shughuli za Bunge. ”
Waziri Mkuu amesema kuwa ni muhimu viongozi hao wakatambua wajibu wa Bunge la Tanzania katika mapambano dhidi ya rushwa kwani rushwa ni adui wa haki, ni kikwazo cha maendeleo, inaathiri mifumo yote ya mahusiano na jamii yetu. “Sisi kama viongozi lazima tuwe kioo kuhakikisha kila kinachopatikana lazima kiende mahali panapotakiwa kifike. ”
Amesema kuwa baada ya mafunzo hayo anaamini viongozi hao watazingatia kikamilifu mipaka yao ya madaraka na utendaji kazi wa Kamati za Bunge na kwamba hatua watakazozichukua katika uongozi na utendaji wao utazingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa wamepata nafasi ya kujifunza kuhusu uongozi wa kimkakati. “Mheshimiwa Waziri Mkuu pia tumepata nafasi ya kukumbushana na majukumu yetu ikiwemo kuhakikisha kila mmoja anakuwa na malengo ambayo ni muhimu kuyafikia na kujiwekea mikakati ya kuyafikia.”