*********************
NA MWANDISHI WETU.
Waziri wa ujenzi na uchukuzi,Prof Makame Mbarawa ameitaka Wakala wa Barabara hapa nchini (TANROADS) kuwa waadilifu katika kusimamia mradi wa ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya 3(Brt 3) kwa viwango walivyokubaliana kwenye mkataba na mkandarasi ili barabara hiyo imalizike kwa wakati.
Prof Mbarawa ameyasema hayo hii leo jijini Dar es salaam katika eneo la Tazara wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 23.3 na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 231 ambao unapita katika barabara ya Nyerere hadi Maeneo ya Gongolamboto.
Amesema Serikali kupitia Wizara hiyo ina mpango mkubwa wa kupunguza misongamano katika miji mbalimbali ambapo Kwa Jiji la Dar es salaam watatengeneza barabara hizo za mabasi yaendayo haraka Kwa awamu 6 ambapo awamu ya kwanza inayoanzia Kivukoni, Gerezani, Morocco Hadi Ubungo Kimara Mbezi na Kibaha umekamilika na unafanya kazi , huku awamu ya pili (brt 2) ya mradi huo kuanzia Mbagala mpaka Gerezani na Kivukoni kupitia barabara ya Kilwa ukitarajiwa kumalizika mwezi April mwaka huu.
Aidha amesema barabara hiyo itakuwa na njia 6 huku akimtaka mkandarasi anayejenga barabara hiyo Kwa kiwango Cha zege ambaye ni Kampuni ya Sino Hydro ahakikishe kazi hiyo inamalizika Kwa wakati.
“kiujumla itakuwa ni barabara ya njia 6 ambapo 3 zitakuwa zinaenda mjini na 3 kuja maeneo ya airpot itakuwa ni barabara nzuri na ya kuvutia na itakuwa na Mataa na tutaweka maeneo mbalimbali Kwa ajili ya kuvukia wananchi hivyo niwaombe wananchi kuwa wavumilivu wakati wa Ujenzi wa barabara hii kutokana na Ujenzi huo kuleta changamoto”alisema Prof Mbarawa.
Aidha Kuhusu ajira Kwa vijana katika mradi huo wa barabara Waziri Prof Mbarawa amemwelekeza mkandarasi huyo Kwa kushirikiana na Tanroad kuwapa kazi vijana ambao wanaajiriwa katika mradi huo kutoka maeneo husika unapopita mradi huo Kwa kuwapa kipaumbele kwani wao ndiyo walinzi wazuri Kwa miradi hiyo.
“popote pale kwenye mradi mtu wa kwanza ambaye anatakiwa kupewa kazi ni wale vijana wanaoishi kwenye maeneo Yale Kwa sababu wao mwisho wa siku ndiyo walinzi wa mradi huo Kwa hiyo naomba Tanroads kaeni na mkandarasi mhakikushe vijana hao mnawapa fursa wanapata kazi ili wawe walinzi wazuri na nichukue fursa kuwataka vijana hao wanaopata kazi kwenye miradi hii wawe waadilifu kwani kumekuwa na changamoto nyingi kwenye miradi yetu, kule Mwanza watu wamekuwa wanaiba vifaa, mafuta pamoja na saruji Kwa hiyo naomba vijana wa Dar es salaam wawe waadilifu na sisi tutawapa fursa kama wanavyoomba”alisisitiza Prof Mbarawa.
Kwa upande wake meneja wa wakala wa barabara (TANROADS) Mkoa wa Dar es salaam Mhandisi Harun Senkuku amesema kuwa Ujenzi wa barabara ya mabasi yaendayo haraka awamu ya 3 unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 20 mpaka kufikia mwaka 2024.
Aidha amesema kuwa (TANROADS) Mkoa wa Dar es salaam itaendelea kuhakikisha pia inayapendezesha maeneo mbalimbali ya barabara katika Jiji hilo Kwa kuzingatia thamani ya fedha iliyowekezwa katika miradi hiyo huku akiwataka wananchi kushirikiana katika kulinda rasilimali ambazo serikali imeweka katika miradi mbalimbali ya barabara.