**********************
Na Mwamvua Mwinyi, Bagamoyo
Feb 27
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amebatilisha,na kutengua umiliki wa shamba namba 934 lililokuwa mali ya AZANIA Investment and management Services Ltd, kitongoji cha Kiembeni Kata ya Mapinga, Bagamoyo Mkoani Pwani ,lenye ukubwa wa hekari 374 na kuamua kulirejesha Serikalini .
Eneo hilo liliingia katika mgogoro mkubwa na wananchi wavamizi ambapo awali AZANIA alitambulika ni mmiliki halali lakini mwishoni mwa wiki Rais Samia ilimpendeza kubatilisha eneo hilo.
Mkuu wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge,akiwa katika muendelezo wa ziara yake kata ya Mapinga, kutatua migogoro iliyokithiri kata ya Mapinga, alieleza kutokana na kutenguliwa kwa umiliki wa AZANIA kitongoji cha Kiembeni, inatafsiriwa wananchi bado ni wavamizi.
“Kwasasa tuendelee kumuombea mh Rais, kwani akiona imempendeza kutoa maelekezo eneo hili kuwa la makazi mtashukuru,lakini kubatilishwa kwake sio uhalali wa kujimilikisha maeneo mliyovamia”
.”Pabaki kama palivyo ndio Maamuzi ya Serikali,msiendeleze kujenga,mtajiingiza katika hatari,muwe na subira “.
Kunenge alieleza kuwa, na endapo kama Rais ataelekeza liwe eneo la makazi litákuwa Halmashauri ili eneo lipangwe.
Mkuu huyo wa mkoa, alifafanua hakuna aliye juu ya sheria, kwa wale wote waliohusika na uuzaji holela na utapeli wa viwanja Mapinga wachukuliwe hatua za kisheria.
“Nimedhamiria kupiga kambi hapa, kuisafisha kata hii, na kukomesha uuzaji holela wa maeneo,kwa kufuata maelekezo ya kamati iliyoundwa na Waziri wa Ardhi Angelina Mabula,na nitahakikisha nayasimamia Maamuzi ya kamati hiyo na Serikali “alieleza Kunenge.
Nae mbunge wa Jimbo la Bagamoyo,Muharami Mkenge alieleza ni wakati wa kufanya maendeleo mengine na atahakikisha migogoro ya ardhi Mapinga na Makurunge inapungua.
Alisema ,Eneo la Greenwood ,lenye ukubwa wa hekari 5,000 pamoja na shamba la JENETA yote yaliyopo Makurunge,sanjali na kiwanja kimoja kilichopo kata ya Kisutu vimerudishwa Serikalini kwa ajili ya shughuli na maelekezo atakayoelekeza Rais.
Mkenge alisema,tangu mwaka 2021 alianza kusimamia kero hizo,na sasa kata ya Makurunge matokeo yameanza kuonekana.
Awali mkuu wa wilaya ya Bagamoyo, Halima Okash alitoa rai kwa Wananchi kuacha kuuza ardhi kiholela na yeyote aliyeuziwa ardhi apate hati ya halali ili kujiepusha na migogoro.
“Huwa nasikiliza kero za wananchi kila Jumanne na Ijumaa na asilimia 99.9 ya malalamiko nayofikishiwa ni migogoro ya ardhi,”hili ni tatizo kubwa katika wilaya yetu na nitahakikisha nalishughulikia “alieleza Okash.
Kwa upande wa wananchi,mzee Bole Shindika alisema msimamo wa Serikali lazima uheshimiwe, wanashukuru Rais kwa hatua ya kwanza aliyoichukua na wanasuubiri muongozo wake.