Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Mariam Nyoka kulia,akikabidhi kwa mganga mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru Dkt Athuman Mkonohumo katikati moja ya kati ya mashuka 30 ili yaweze kuboresha huduma zamatibabu katika Hospitali hiyo.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani Ruvuma Dkt Athuman Mkonohumo kulia akipokeaa vifaa tiba vya kupima ugonjwa wa sukari na magonjwa yasioambukiza kutoka kwa Mbunge wa viti maalum Mariam Nyoka.
***************************
Na Muhidin Amri,
Tunduru
MBUNGE wa viti maalum mkoa wa Ruvuma(CCM) Mariam Nyoka,ametoa msaada wa vifaa tiba mbalimbali katika Hospitali ya wilaya Tunduru mkoani humo ikiwa ni kutimiza azima yake ya kupunguza baadhi ya changamoto zilizopo katika Hospitali hiyo na kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya.
Vifaa vilivyotolewa ni mashuka 30 na chandarua 15 kwa ajili ya wodi ya akina mama,mashine za kupimia magonjwa yasioambukiza(BP na Sukari) kwa wananchi watakaofika kupata huduma ya matibabu katika Hospitali hiyo.
Akizungumza baada ya kukabidhi vifaa hivyo Nyoka alisema, msaada huo unatokana na dhamira yake ya muda mrefu kabla hajawa Mbunge kwa kutoa kile alichonacho kuisaidia jamii yenye shida na kuunga mkono jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali kuhakikisha nchi yetu inakuwa na watu wenye afya bora.
Alisema,kipaumbele chake cha kwanza kama Mbunge wa vitu maalum ni kusaidia katika sekta ya afya kwa kuwa sekta hiyo ni moja ya nguzo kuu na yenye mchango mkubwa katika kuleta mabadiliko ili kuwa na watu wenye afya njema, wenye uwezo wa kufanya kazi za kujiletea maendeleo yao na kushiriki kukuza uchumi wa mkoa wa Ruvuma nchi yetu.
Nyoka,amewakumbusha watoa huduma katika Hospitali hiyo na sekta yote ya afya mkoani Ruvuma,kutoa huduma bora kwa wananchi bila kubagua kwani ni sehemu muhimu na wajibu wao.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi Dkt Athuman Mkonohumo, amemshukuru Mbunge huyo kwa kutoa vifaa tiba ambavyo vitakwenda kuboresha huduma za afya na kuongeza juhudi za serikali za kuboresha huduma za afya katika Hospitali hiyo.
Dkt Athuman alisema,vifaa hivyo vitawasaidia watumishi kutekeleza vyema majukumu yao ya kila siku na wananchi kupata huduma bora za matibabu.
Pia,ametoa wito kwa mashirika,taasisi ,wadau na viongozi wengine wenye uwezo,kujitokeza na kuisaidia Hospitali kwani bado inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo upungufu wa vitanda na vifaa vingine kwa ajili ya kuboresha utoaji huduma za afya.
Muuguzi mfawidhi wa Hospitali hiyo Nelly Simon amesema,vifaa hivyo vinakwenda kusaidia na kuboresha suala zima la matibabu katika Hospitali hiyo ambayo inakabiliwa na idadi kubwa ya wagonjwa.
MWISHO.