SEHEMU ya wajumbe wa Baraza hilo wakifatilia mada mbalimbali wakati wa uzinduzi wa Baraza la Biashara Mkoa huo lililozinduliwa Februari 25,2023 jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
MKUU wa Mkoa wa Dodoma Mhe.Rosemary Senyamule,amewataka wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa ngazi ya wilaya kwenda kutenga maeneo ya uwekezaji ambayo yatavutia wageni kuwekeza katika halmashauri zao.
Hayo ameyasema Februari 24,2023 jijini Dodoma wakati wa uzinduzi wa Baraza la Biashara Mkoa huo lenye mpango mkakati wa kuifanya Dodoma kwa kitivo cha Biashara na Uwekezaji nchini.
RC Senyamule amesema kuwa Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuleta wawekezaji kutoka nje na wanaingia kwa wingi nchini hivyo lazima mkoa na halmashauri zake zikatenge maeneo ambayo yatakuwa rafiki kwa wawekezaji pindi watakapokuja kuwekeza.
”Mkoa wa Dodoma tunataka tuwe na mchango Mkubwa kwenye Biashara hivyo ni matarajio yangu Baraza la Mkoa litakua bora na lenye utashi wa kipekee kwenye makao makuu ya nchi
”Hivyo nawaomba wajumbe wa Baraza hilo ngazi ya wilaya kwenda kufanya vikao vya mabaraza pamoja na wale wa Halmashauri, Wakurugenzi nao wakafanye hivyo,pia muende mkatenge maeneo ya uwekezaji ambayo yatavutia wageni watakapohitaji kwenda kuwekeza kwenye Halmashauri zenu. ”amesema RC Senyamule
Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Dodoma Dkt. Fatuma Mganga,amesema kuwa lengo la Baraza hilo ni kuifanya Dodoma kuwa kitovu cha Biashara nchini .
”Malengo madogo yakiwa ni kuwa na mpango mkakati wa kufanya kazi ndani ya miaka mitatu, kutangaza shughuli za Biashara na fursa za uwekezaji kupitia vyombo vya biashara, kuongeza idadi ya uwekezaji unaofanyika Dodoma, maeneo ya uwekezaji yaliyotwaliwa yapimwe ili yaboreshwe, mabaraza ya Wilaya yaboreshwe pamoja na kuongeza wafanyabiashara” amesema Dkt. Mganga