Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akioneshwa eneo la mradi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja la Mto Mkavu na Likong’o katika manispaa ya Lindi na Mpima wa manispaa hiyo Kisna Mgeni (kushoto) wakati wa kupatiwa taarifa ya mradi huo Ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akitoa ufafanuzi kwa timu ya wataalamu waliokwenda ofisni kwake jijini Dar es Salaam kumpa taarifa ya mradi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja la Mto Mkavu na Likong’o unaotekelezwa na Manispaa ya Lindi
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akipitia taarifa ya mradi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi wakati timu ya wataalam ilipokwenda kumpa taarifa ya mradi huo ofisini kwake jijini Dar es Salaam
Sehemu ya wataalamu waliokwenda ofisini kwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula jijini Da es Salaam kumpa taarifa ya mradi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo la Mto Mkavu na Likong’o wakifuatilia uwasilishaji taarifa ya mradi
Mpima wa Manispaa ya Lindi Mkoani Lindi Kisna Mgeni akiwasilisha taarifa ya mradi la kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi mbele ya Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi tarehe 23 Februari 2023 katika ofisi ndogo ya Wizara jijini Dar es Salaam.
Afisa Mipango Miji kutoka Kampuni ya Ardhi Solution Ramadhani Hamis akimuonesha Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula kupitia ramani ya maeneo ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi tarehe 23 Februari 2023 jijini Dar es Salaam.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesisitiza maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya shughuli za uwekezaji nchini kupangwa, kupimwa na kumilikishwa kwa lengo la kuepuka migogoro ya ardhi.
Dkt Mabula ametoa kauli hiyo tarehe 23 Februari 2023 katika ofisi ndogo ya Wizara ya Ardhi jijini Dar es Salaam wakati akipewa taarifa ya mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja eneo lenye ukubwa wa ekari 630 lililopo mkabala na mradi wa kuchakata gesi asilia-LNG la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi unaotekelezwa na halmashauri ya manispaa ya Lindi.
Waziri Mabula alisema, katika kipindi hiki ambacho Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan anasisitiza suala la uwekeza ni muhimu mamlaka husika kuhakikisha zinapanga, kupima na kumilikisha maeneo ya uwekezaji ili kuwarahisishia wawekezaji wanapokuja kuwekeza nchini.
Akielezea zaidi kuhusu mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja katika eneo la Mto Mkavu na Likong’o mkoani Lindi Dkt Mabula pamoja na kupongeza mradi huo ametaka kuwepo uwazi wakati wa mchakato mzima wa kutangaza viwanja vya mradi huo sambamba na kuepuka mtu mmoja kuchukua viwanja vingi ambavyo mwisho wa siku atashindwa kuviendeleza kwa wakati.
‘’Hatuzuii mtu kuchukua viwanja lakini siyo mtu achukue mtaa mzima halafu anashindwa kuviendeleza na eneo kubaki vichaka, mimi sitotaka kusikia jambo hilo katika kipindi changu cha uongozi hapa wizara ya ardhi’’ alisema Dkt Mabula.
Aidha, Waziri wa Ardhi ameitaka Halmashauri ya Manispaa ya Lindi kuharakisha mradi huo huku akisisitiza mradi kujumuisha maeneo yote muhimu kama vile mahoteli, huduma za kijamii, viwanja vya mpira na gofu, maeneo ya kupumzikia, shule, huduma za afya pamoja na maeneo ya viwanda.
Kupitia mradi wa kupanga, kupima na kumilikisha viwanja, halmashauri ya Manispaa ya Lindi imelenga kupanga na kupima viwanja visivyopungua 3,000 vyenye matumizi mbalimbali yenye sura ya kiuwekezaji kutokana na mpango wa mipangomiji ulivyoanishwa na kukubalika kulingana na mpango wa matumizi.
Akiwasilisha mpango huo mbele ya Waziri Dkt Mabula, Mpima wa Manispaa ya Lindi Kisna Mgeni alisema, halmashauri kwa kuzingatia mpango wa mipangomiji inategemea eneo la mradi kuwa na wakazi 13,000 na kuzalisha takriban ajira 5,400 kutokana na huduma mbalimbali za viwanda, biashara, huduma za afya, usafirishaji pamoja na huduma za elimu kwenye eneo hilo.
Kwa mujibu wa Kisna mbali na eneo la mradi kuwa la serikali lakini kuna baadhi ya wananchi wamefanya maendelezo kwa kuweka makazi na shughuli za kilimo kwa kumiliki mazao ya kudumu.
Alisema, kutokana na azma ya halmashauri yake kuhakikisha wananchi wote wenye makazi Mtomkavu pamoja na Likong’o wanamiliki maeneo yao kisheria, tayari halmashauri hiyo imepokea maombi ya kurasimishiwa makazi wananchi wote hivyo eneo la ekari 293 nje ya eneo la serikali limeongezeka na kufanya mradi kuwa na eneo lenye ukubwa wa ekari 923.5.
‘’Halmashauri imefanya uthamini wa mazao ya kudumu na kuacha makazi ya wakazi waliopo ndani ya mradi kwa makubaliano ya kuendelea kuwapa wananchi wa mtomkavu na Likong’o fursa ya kumiliki ardhi iliyopo karibu na mradi wa kuchakata gesi asilia (LNG)’’ alisema Kisna.
Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ilipokea mkopo wa shilingi Bilioni Moja na Milioni Mia Tano (1,500,000) toka Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa ajili ya kupanga, kupima na kumilikisha viwanja kwenye eneo la Mtomkavu na Likong’o eneo lililopo mkabala na mradi mkubwa wa kuchakata Gesi Asilia –LNG.