MKURUGENZI wa Bodi ya huduma za Maktaba Zanzibar Ndg.Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim,akizungumzia huduma mbalimbali zinazotolewa na maktaba kuu Zanzibar katika kipindi cha Safari ya Bahari ninachorushwa na Kituo cha Radio Bahari FM.
**************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
MKURUGENZI wa Bodi ya huduma za Maktaba Zanzibar Ndg.Ulfat Abdul-Aziz Ibrahim, amewasihi wazazi na walezi nchini kuwa makini wakati wanaponunua vitabu vya watoto kwa ajili ya kusomea.
Nasaha hizo amezitoa wakati akizungumzia masuala ya kiutendaji juu ya huduma za maktabar nchini kupitia kipindi cha safari ya Bahari kinachorushwa na radio Bahari FM huko iliyopo Migombani Zanzibar.
Alisema kuna baadhi ya vitabu na machapisho yanayouzwa katika maeneo mbalimbali hayaendani na desturi,mila na maadili ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Katika maelezo yake Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kila mwananchi ana jukumu la kulinda maadili na utamaduni wa nchi yake na kwamba watoto wanahitaji uandalizi wa kipekee katika malezi ya kila siku.
Alieleza kuwa katika taasisi hiyo wanaendelea kukagua kwa kina maktaba za skuli za umma na binafsi ili kubaini vitabu na machapisho yanayokiuka maadili yanaondolewa katika taasisi hizo.
“Kila mwananchi achukue juhudi za kulinda watoto bila kujali mtoto ni wa nani na anafanya nn kwani changamoto zipo nyingi katika masuala ya kusoma vitabu ni muhimu kabla hatujawanunulia watoto wetu tujiridhishe kwanza kama vionaendana na maadili yetu”,.alisema Ulfat.
Aidha alisema kuwa changamoto hizo zimebainika katika vitabu vya lugha ya kiengereza vinavyochapishwa na makampuni ya nje ya nchi.
Pamoja na hayo aliendelea kuwasihi wananchi kuendeleza utamaduni wa kutembelea maktaba kusoma vitabu na machapisho mbalimbali kwa lengo la kupata taarifa na maarifa.
Naye Mkuu wa Divisheni ya huduma za maktaba Zanzibar Mahfudha Abdallah Abdulkadir,amewataka wananchi kuwapeleka watoto katika maktaba kuu ili wasome vitabu mbalimbali na uwezo wao wa kitaaluma.