Kaimu Afisa elimu sekondari wa Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma Rashid Bundala kulia,akizungumza na baadhi ya wanafunzi na walimu wa shule ya sekondari ya wasichana Mbinga(Mbinga Girls) jana
Baadhi ya vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya wasichana Mbinga vilivyojengwa kwa fedha za mpango wa maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Uvico-19.
**************************
Na Muhidin Amri, Mbinga
WANAFUNZI wa shule ya sekondari ya wasichana Mbinga wamesema,kujengwa kwa vyumba vipya vya madarasa vimewaongezea ari ya kujisomea na kuhaidi watavitumia kusoma kwa bidii ili waweze kufanya vizuri katika masomo yao.
Wameishukuru serikali kuwajengea vyumba vipya vya madarasa ambavyo vimesaidia kupunguza msongamano na kuongeza utulivu madarasani wakati wa kujisomea.
Wamesema hayo jana wakati wakizungumza na HABARILEO, juu ya ujenzi wa miumbombinu ya elimu iliyotekelezwa na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wake.
“tunamshukuru sana mama yetu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutujengea vyumba vipya vya madarasa na mabweni katika shule yetu,kwa sasa tunasoma kwa amani na utulivu mkubwa,hapo awali wenzetu waliotangulia katika shule hii walikutana na changamoto kubwa ya msongamano darasani ambao sasa haupo tena”alisema mwanafunzi wa kidato cha nne Uwezo Komba.
Komba alieleza kuwa,ujenzi wa madarasa mapya sambamba na viti na meza umehamasisha hata wanafunzi wanaopelekwa katika shule hiyo kufurahi mazingira mazuri na kupenda shule tofauti na hapo awali ambapo wazazi walilazimika kwenda na vifaa ambavyo sasa mwanafunzi anavikuta shuleni.
Debora Mapunda amesema,tangu walipofika katika shule hiyo wamefurahia mazingira ya shule kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu uliofanywa na serikali ya awamu ya sita na kuhaidi kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu.
Nuru Ibrahim mwanafunzi wa kidato cha nne amesema,kabla ya ujenzi wa vyumba vipya vya madarasa kero kubwa ilikuwa ni msongamano wa wanafunzi kwani darasa moja lilikuwa na wanafunzi kati ya 40 na 45,hivyo kukosa na utulivu na kushindwa kusikiliza yanayofundishwa na walimu.
Aidha,ameishauri serikali kuendelea kuwekeza kwenye ujenzi wa mabweni na kujenga wigo(uzio) kuzunguka eneo lote la shule na viwanja vya michezo ili waweze kushiriki michezo mbalimbali hasa ikizingatiwa kuwa kwa sasa michezo ni ajira.
Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo Theresia Mlwilo, ameishukuru serikali kwa kutoa jumla ya shilingi milioni 40 kwa ajili ya kujenga vyumba viwili vya madarasa ambavyo vimesaidia sana wanafunzi kuwa na sehemu nzuri ya kujifunzia na walimu kufundishia.
Amesema,madarasa mapya yamaechochea wanafunzi wa shule hiyo kupenda kusoma,hata hivyo ameiomba serikali kuongeza nguvu katika ujenzi wa mabweni kwani yaliyopo hayakidhi mahitaji kutokana na idadi kubwa ya wanafunzi.
Naye Mwalimu wa taaluma Richard Mhuwa amesema,katika shule hiyo walipangiwa kupokea wanafunzi 100 wa kidato cha kwanza na wote wameripoti kwa ajili ya kuendelea na masomo ya sekondari.