**************************
Na. Mwandishi wetu Jeshi la Polisi
Wafugaji wote Nchini wametakiwa kufuata taratibu ikiwemo kutafuta vibali ama barua toka kwa viongozi wa serikali za vijiji kabla ya kupeleka mifugo yao kwenye minada ili kuondoa mashaka toka kwa wakaguzi wa mifugo.
Hayo yamesemwa leo februari 22, 2023 na Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo Nchini Kamishna Msaidizi wa Polisi ACP Simon Pasua wakati akizungumza na Wafugaji pamoja na wafanyabiashara wa mifugo katika mnada wa Duka bovu uliopo wilaya ya Monduli mkoani Arusha.
ACP Pasua amesema jeshi hilo linatoa elimu katika minada yote nchini ambayo ipo zaidi ya 530 na kubainisha kuwa kupitia elimu hizo pamoja na mambo mengine wafugaji wanaelimishwa taratibu za kufuata za namna bora ya kuuza mifugo yao kuepusha migogoro.
Sambamba na hilo pia amewataka wafugaji wote nchini kuzingatia matumizi sahihi ya ardhi ili kuepuka migogoro baina yao na watumiaji wengine wa ardhi hususani ile iliyotengwa kwa ajili ya kilimo.
Kamanda Pasua ameendelea kusema kupitia elimu hiyo ni imani yake kuwa wafugaji wote watabadilika na kufuata taratibu zote zinazohitajika za usafirishaji wa mifugo na kuwataka kutoa ushirikiano kwa jeshi hilo ili kuhakikisha mifugo inaendelea kuwepo.
Kwa upande wake bwana Kirayani Laizer ambaye ni mfugaji amesema njia bora ya kudhibiti mifugo ya wizi ni pale ambapo kutawekwa utaratibu wa kuzuia mifugo yote ambayo haina vibali toka kwa balozi au viongozi wa vijiji kuingia minadani.
Pia amewataka wafugaji wote kuhakikisha wanafuata taratibu na kanuni za kuuza mifugo yao ikiwemo kutafuta vibali toka kwa mamlaka zote zinahusika ili kuepukana na migogoro.
Naye bwana Babug Ngoti ambaye ni mfanyabishara wa mifugo ametoa wito kwa wafanyabiashara wenzake kuhakikisha wanafanya biashara yenye kuleta uwiano mzuri baina ya wafanyabishara, wafugaji pamoja na serikali.