Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi nakala ya Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039 Meya wa jiji hilo Dourmohamed Issa katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo tarehe 21Februari 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati), Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera (kushoto) na Meya wa jiji la Mbeya Dourmohamed Issa wakiwa wameshika nakala za Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039 uliozinduliwa katika hafla iliyofanyika tarehe 21Februari 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akikata utepe kuzindua Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039 katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo tarehe 21Februari 2023.
Afisa Mipango wa jiji la Mbeya Arafa Ismail akitoa ufafanuzi katika Ramani ya Mpango Kabambe wa jiji hilo 2019-2039 wakati wa hafla ya uzinduzi wa mpango huo tarehe 21Februari 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi nakala ya Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039 Kamishna wa Ardhi Msaidizi Mkoa wa Mbeya Siyabumi Mwipopo katika hafla ya uzinduzi wa mpango huo tarehe 21Februari 2023.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiwasili viwanja vya Kabwe mkaoni Mbeya kwa ajili ya kuzindua Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039. Kulia ni Mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera na kushoto ni Meya wa Jiji la Mbeya Dourmohamed Issa.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akisalimiana na viongozi wa kimila alipowasili kwa ajili ya kuzindua Mpango Kabambe wa Jiji la Mbeya 2019-2039.(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Na Munir Shemweta, WANMM MBEYA
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amezindua Mpango Kabambe wa jiji la Mbeya 2019-2039.
Uzinduzi wa Mapngo huo umefanyika leo tarehe 21 Februari 2023 na kuhudhuruwa na viongozi mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, madiwani , wakurugenzi wa halmashauri na wakuu wa taasisi za serikali.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Dkt Mabula alisema lengo kuu la kuandaa mpango kabambe wa jiji la mbeya ni kutoa dira ya namna jiji la Mbeya litakavyopaswa kukua na kuendelezwa kwa kipindi cha miaka 20 kuanzia 2019-2039.
‘’Mpango huu unaanisha mikakati ya uendelezaji na uboreshaji maeneo ya zamani yaliyojengwa kiholela kama vile sehemu za maeneo ya kata ya Sinde, Mahanga, Mabatini, Forest ya Zamani, Ilomba na Simike na maeneo kongwe yaliyochakaa sana’’ alisema Dkt Mabula.
Mpango Kabambe uliozinduliwa umetaja mikakati minne ya kusimamia ukuaji na maendelezo ya jiji la Mbeya ambayo ni uendelezaji upya maeneo kongwe, kurasimisha makazi ambayo kimipangomiji hayajaathirika sana lakini kuna uwezekano wa kupata miundombinu, kusimamia yasiyoathirika kwa kuvamiwa na ujenzi holela pamoja na mkakati wa kuanzisha miji ya pembezoni.
Dkt Mabula ametoa wito kwa taasisi zinazotoa huduma mbalimbali kwenye jiji la Mbeya kuutumia Mpango Kabambe ulioandaliwa katika utekelezaji wa shughuli zao na miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha, amemuelekeza mkuu wa mkoa wa Mbeya Juma Homera kuunda timu maalum itakayosimamia utekelezaji Mpango Kabambe wa jiji la Mbeya na wajumbe wake watoke katika taasisisi zote zinazowajibika kutekeleza miradi mbalimbali iliyoanishwa katika mpango huo.
Alisema, katika awamu ya sita chini ya uongozi wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, uwekezaji katika viwanda na ujenzi wa miundombinu unatiliwa mkazo na msukumo mkubwa hivyo utayarishaji wa mpango kabambe ni hatua muhimu sana kufikia azma hiyo.
Aliongeza kwa kusema katika kufikia azma hiyo wizara ya ardhi imekuwa ikisisitiza kila mamlaka ya upangaji kuandaa mpango kabambe wa eneo lake ili kuendana na kasi ya utekelezaji wa azma hiyo na kuvutia wawekezaji.
Kwa mujibu wa Dkt Mabula kwa kushirikiana na na mamlaka za upangaji jumla ya mipango kabambe 26 imekwisha idhinishwa na wizara ya ardhi ambapo kati ya hiyo 6 ni ya majiji ikiwemo jiji la mbeya, 13 katika manispaa na 7 katika halmashauri za miji.
Ametoa rai kwa mamlaka za upangaji nchini kuandaa mipango kabambe ya maeneo yao kwa kutumia wataalamu washauri au wataalamu wa ndani kadri ya uwezo wa mamlaka ya upangaji.