Na Lucas Raphael,Tabora
Serikali imeipatia vifaa vya kisasa Hospitali ya wilaya ya urambo mkoani Tabora kwa ajili ya uchunguzi wa magonjwa ya moyo,ini na figo lengo likiwa ni kusongeza huduma za matibabu karibu na wananchi .
Kabla ya kupatiwa vifaa hivyo huduma hiyo ilikuwa inapatikana katika mijini ya Tabora , Igunga na Bugando mkoani Mwanza kwa ajili ya kufuata upimaji wa magonjwa hayo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisni kwake jana Mganga mkuu wa wilaya ya urambo Dkt David Manyama alisema kwamba kupatikana kwa vifaa hivyo vimerahisisha huduma kwa wananchi wa wilaya hiyo ambao walikuwa wanapata usumbufu wa kufata upimaji wa afya mbali na wilaya hiyo.
Alisema kwamba serikali ya awamu ya sita ilitoa fedha kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya kisasa vyenye uwezo wa kupima magonjwa makubwa ya moyo,ini na figo jambo ambalo litasaidia wananchi wilayani humo kupata huduma za matibabu karibu na kuokoa gharama kubwa amabyo wamekuwa wakikutana nayo kwa muda mrefu
Dkt Manyama alisema kwamba hospitali hiyo ilipokea kiasi cha shilingi million 300,000,000 kwa ajili ya ujenzi wa jengo la dharura na mashine ya mionzi (x-rey mashine) iliyogharimu Zaidi ya shilingi million 150,000,000.
“Tunaishukuru serikali kwa kutoa fedha za ujenzi wa jengo la dharura na ununuzi wa vifaa tiba vya kisasa jambo litalosaidia kutoa huduma bora kwa wananchi” alisema Dkt Manyama .
Aidha alisema kwamba wataendela kuishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwani kwa sasa miundombinu ya majengo na vifaa tiba vya kutolea huduma za afya katika hospitali hiyo imeimarika kwa kiasi kikubwa kutokana na kupokea vifaa hivyo.
Dkt Manyama alisema kwamba wanatarajia kutoa huduma kwa wilaya ya urambo wilaya na jirani ikiwemo Kaliua, Uyui na Sikonge na mikoa za jirani ikiwemo mkoa wa Kigoma na Katavi kutokana na ukubwa wa huduma zinazotolewa katika hospitali hiyo.
Kwa upande wao watoa huduma za afya katika hospitali hiyo Matias Masheli na Costantine Ngoile walisema awali kabla ya kuboreshwa kwa miundombinu ya afya na kuletwa kwa vifaa hivyo walikuwa wakifanya kazi kwenye mazingira magumu lakini kwa sasa wanaishikuru serikali kwa kufanya maboresho hayo jambo linalowafanya watoe huduma kwa wakati.
Wananchi wilayani humo walikuwa wakipata shida kwenda mbali kufuata huduma ambazo kwa sasa zinatolewa hospitalini hapo ambapo jengo jipya la dharura limetengezwa kwa mfumo ambao unaweza kutoa taarifa ya maendeleo ya mgonjwa na mabadiliko ya hali yake moja kwa moja kwa watoa taarifa kupitia mashine zilizopo katika jengo hilo.