Na Mwamvua Mwinyi ,Pwani
MKUU wa mkoa wa Pwani alhaj Abubakari Kunenge, ametoa rai kwa kamati ya hamasa na mawasiliano dhidi ya magonjwa ya mlipuko ,wakati inajengewa uwezo katika majukumu yao iweke mpango kazi kushughulikia changamoto kubwa ya ukatili na unyanyasaji ikiwemo kwa wanawake na watoto Mkoani humo.
Akifungua kikao kazi cha kuwajengea uwezo kamati ya hamasa na mawasiliano dhidi ya magonjwa ya mlipuko (RCCE) ,Mkoa na wasilisho la muundo wa kamati hiyo Mkoa na Halmashauri sanjali na majukumu yao, Kunenge alieleza, Mkoa huo bado una shida ya suala la unyanyasaji na udhalilishaji kwa kundi hilo.
Vilevile, aliitaka jamii kuchukua tahadhari za kukabiliana na magonjwa ya Mlipuko ikiwemo Covid 19, Kipindupindu, Ebola, Kimeta na mengineyo kutokana na hatari kubwa ya kusababisha vifo.
Pia, aliipongeza Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na shirika la afya Duniani (WHO) kwa jitihada kubwa wanazozifanya za kukabiliana na magonjwa hayo hatari katika jamii ikiwemo kudhibiti magonjwa ya mlipuko.
Alieleza,baada ya mafunzo hayo kamati hiyo wafuate mfumo wa kutoa ushirikishwaji wa jamii ili kuondoa tatizo la magonjwa ya mlipuko na unyanyasaji na udhalilishaji .
“Tatizo hili bado ni kubwa, natambua majukumu ya kamati yatafanyiwa kazi Lakini na changamoto ya udhalilishaji na unyanyasaji lisimamiwe ili kupambana nalo kwenye jamii”alieleza Kunenge.
“Hili ni jambo jema kimkoa la kimkakati, limekuja wakati muafaka kwani uwekezaji upo kwa kasi viwanda sasa vimefikia 1,420 kati ya hivyo vikubwa 97, uwekezaji unaenda kwa kasi na Wakazi ni wengi, idadi inaongezeka kila siku,ni vyema magonjwa ya mlipuko kudhibitiwa kama tutatumia mfumo wa mawasiliano, na kila penye changamoto pafikiwe, malengo tarajiwa yatafikiwa”alifafanua mkuu huyo wa mkoa.
Mkoa upo makini tunapofanya kitu tufanye kwa uhakika wa kutoa matokeo chanya, na tutafanikiwa.