Mkuu wa chuo cha Shirikisho la mifuko ya hifadhi ya jamii katika nchi za Afrika Mashariki na kati (ECASSA),Emmanuel Magoti akizungumza na waandishi wa habari.
***************************
Julieth Laizer ,Arusha
Arusha.Wananchi wametakiwa kuunga mkono azma ya serikali ya kuleta Bima ya Afya ya Taifa kwa wote kwani inasaidia sana kutatua changamoto za afya kwa watu wote, kwa usawa na kwa wakati bila kujali hadhi au kipato cha mtu.
Hayo yamesemwa leo jijini Arusha na Mkuu wa Chuo Cha Shirikisho la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii katika nchi za Afrika Mashariki na kati(ECASSA) , Emmanuel Magoti wakati akizungumza kwenye mafunzo ya kuwajengea uwezo wafanyakazi wa mifuko ya hifadhi ya jamii kutoka nchi saba za Afrika Mashariki na Kati kuhusu namna bora ya kiutawala na kiutendaji ya kuendesha na kusimamia mifuko ya kijamii na kitaifa ya bima ya afya kama njia ya kufikia malengo ya huduma nafuu ya afya kwa jamii nzima pasipo kubagua makundi yasiyokuwa na uwezo.
Magoti amesema kuwa, mafunzo hayo yenye mada kuu ya Bima ya Afya ya Kitaifa kwa Makundi Yenye Kipato Kidogo na Yale Yasiyojiweza Kiuchumi Kama Njia Mbadala ya Kufikia Malengo ya Huduma za Afya Kwa Wote yanalenga kutoa elimu kwa bodi za wakurugenzi, menejimenti na wafanyakazi wa mifuko ya taifa ya bima ya afya katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati .
Amesema kuwa, wanapewa mafunzo namna ya kusimamia mifuko hiyo kwa ufanisi na namna ambavyo bima hiyo inaweza kufikia lengo la kitaifa la bima ya afya kwa wote na lengo namba 3 la malengo 17 ya maendeleo endelevu duniani ( Sustainable Development Goals) ya 2030, ambalo ni “Afya na Ustawi kwa watu wote, pasipo kumwacha hata mmoja nyuma.
Amesema kuwa, Bima ya Taifa ya Afya ina manufaa makubwa sana kwani hazinaga ukomo wa matibabu na ukiumwa unatibiwa katika hospitali na vituo vya afya hadi upone au hadi mauti yakitokea.
“Mkakati wa Umoja wa Mataifa ni kuhakikisha kwamba ifikapo mwaka 2030 nchi zote duniani ziwe zimefikia lengo la kutoa huduma ya Afya bure au kwa gharama nafuu kwa raia wake wote ili kuweza kufikia kauli mbiu ya afya kwa wote,hili linaweza kufikiwa katika ngazi ya nchi endapo tu kuna mfumo thabiti wa Bima ya Taifa ya Afya.”amesema Magoti.
Amesema kuwa, ECASSA inahudumia jumla ya mifuko 19 ya Hifadhi ya Jamii ambao ni wanachama wake kutoka nchi 7 za Mashariki na Kati mwa Afrika ambazo ni Tanzania ,Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia na Zimbabwe ambapo makao makuu ya taasisi hiyo yalikuwa Nairobi Kenya kabla ya kuhamia Arusha Tanzania mwaka 2016 ili kuweza kufanya shughuli zao kama sehemu ya utekelezaji wa ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kama taasisi ndani ya nchi hizi.
Magoti amefafanua kuwa,lengo la serikali ya Tanzania kupeleka muswada wa Sheria ya Bima ya Afya wa 2022 Bungeni na baadae kuwa sheria itakayopelekea haki ya kikatiba ya Bima ya Afya kwa Watanzania wote, ukiwemo utaratibu maalumu wa uchangiaji ili kumwezesha hata yule mwenye kipato kidogo kuweza kuchangia kiasi fulani kidogo.
Ameongeza kuwa ,malengo mengine ni kuhakikisha kwamba hatimaye watanzania wote bila kujali umri, jinsia, elimu au kipato cha mtu, wanapata matibabu nafuu na kuwaepusha na gharama kubwa za matibabu ambazo ni mzigo kwa familia duni ambazo mara nyingi hutumbukia katika umasikini zinapolazimika kujilipia matibabu kutoka mifukoni mwao,ni hatua ya kupongezwa ya serikali inayopaswa kuungwa mkono na watanzania wote.
Magoti amefafanua kwamba, nguvu kazi ya taifa iliyo katika afya bora itokanayo na kuwa na uhakika wa matibabu nafuu mahali popote nchini kwa njia ya Bima ya Taifa ya Afya, huongeza tija katika uchumi na kupunguza au kuondoa kabisa umasikini.
“Sisi ECASSA tunatamani sana kupata fursa ya kuweza kuelezea umuhimu wa Bima za Afya za Kitaifa kwa watanzania wote tuweze kuwaelemisha wananchi kwa ufasaha faida kubwa sana hususani za kiafya na kiuchumi zitakazotokana na wao kupata Bima ya Afya inayotolewa na serikali ya Tanzania ambapo wao wananchi wananchangia kiasi fulani tu cha pesa kwa mwaka, lakini wanapata matibabu pasipo ukomo na utaratibu unaoweza kufanyika kwa ajili ya makundi maalum . Hii ni elimu muhimu wananchi kupewa, hususani katika kipindi hichi ambapo serikali imepeleka muswada huu wa Bima ya Afya kwa Wote 2022 Bungeni.