Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka baada ya upelelezi kukamilika limefanikiwa kumfikisha mahakamani mkazi mmoja (46) wa Sombetini Jijini Arusha kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake (Jina limehifadhiwa) (07) mwanafunzi wa darasa la kwanza.
Aidha pamoja na uwepo wa tukio hilo lakini pia kwa kipindi cha mwezi Januari 2022 hadi Januari 2023 jumla ya watuhumiwa 241 walipatikana na hatia na kuhukumiwa kwenda jela vifungo mbalimbali kwa makosa ya ulawiti na ubakaji.
Tarehe 16.02.2023 Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha ilimhukumu mtu mmoja aitwaye KELVIN WILFRED (19) mkazi wa Muriet Arusha kwenda Jela kifungo cha Maisha kwa kosa la kumbaka mwanafunzi (jina limehifadhiwa) (08) wa darasa la Nne.
Wakati huo huo Mahakama ya wilaya ya Karatu, Arumeru na Monduli ziliwahukumu PETER LEONARD (27) mkazi wa Lashaine Monduli, PAUL HILONGA (60) mkazi wa Karatu, JOHN SANARE (24) mkazi wa Arumeru kwenda Jela vifungo vya maisha kila mmoja kwa makosa ya Ubakaji na ELIASI NDASIKOI (23) mkazi wa Arumeru naye alihukumiwa kifungo cha maisha kwa kosa la Kulawiti.
Wengine waliohukumiwa na Mahakama ya Wilaya ya Arumeru na Karatu vifungo vya miaka 30 kila mmoja kwa makosa ya ubakaji ni JAMES ELIREHEMA mkazi wa Maloloni ELIAS ROBERT (27) mkazi wa Ambureni, JAPHET MUNGURE wote wa wilaya ya Arumeru na THEOPHILI SALAHO (32) mkazi wa kijiji cha Chanoldean wilayani Karatu.
Sambamba na hilo pia kwa kushirikiana na vyombo vingine vya serikali tutaendelea kufuatilia kwa mujibu wa sheria wale wote watakaobainika kutenda matukio ya uhalifu ikiwemo ya ukatili na unyanyasaji katika jamii.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha tunawashukuru wadau mbalimbali ikiwemo wazazi, viongozi wa Dini, viongozi wa kimila na Waandishi wa Habari kupitia dhana nzima ya ushirikishwaji wa jamii na kupitia program ya Polisi jamii kuhusiana na kuzuia ukatili wa kijinsia ambayo imepekelekea jamii kuacha kuficha matukio ya ukatili badala yake wanayaibua na kuripoti matukio mengi yanayotokea.
Pia tunatoa wito kwa wazazi na walezi, viongozi wa dini, mila, serikali pamoja na wadau wengine kuendelea kutoa elimu pamoja na kukemea vitendo vya mmomonyoko wa maadili katika jamii ambao unapelekea kuongezeka kwa matukio hayo.
Sambamba na hilo pia tunawaomba wananchi kuendelea kufichua matukio ya uhalifu katika jamii ili tuweze kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaobainika.
Tukio la Ajali ya Pikipiki iliyosababisha vifo vya watu.
Tarehe 15.02.2023 muda wa saa 01:00 jioni huko maeneo ya Momela, Wilaya ya Arumeru katika Barabara ya Moshi – Arusha gari lenye namba za usajili T. 493 BJR aina ya Corona Premio likiendeshwa na Dereva aitwaye ALLY IDD (45) mkazi wa Maji ya Chai liligongana na pikipiki ikiendeshwa na dereva aitwaye ELISHA ANTHONY ikiwa imepakia watu watatu na kusababisha vifo kwa watu wawili pamoja na majeruhi wanne ambapo katika ajali hiyo pikipiki mbili zilihusika.
Waliofariki katika ajali hiyo ni ELISHA ANTHONY (25) Dereva pikipiki pamoja na PIUS CALIST TARIMO (17) dereva wote wakiwa ni wakazi wa Sokoni One Jijini Arusha. Marehemu PIUS CALIST LAZARO yeye alifariki dunia tarehe 17.02.2023 wakati anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mount meru Arusha.
Aidha waliojeruhiwa ni PAULO HENRY (20) mkazi wa Sokoni One, SAIDI ELIAS (23) mkazi wa Uswahilini walipatiwa matibabu na kuruhusiwa. Majeruhi wengine ambao ni EMMANUEL JOHN (18) mkazi wa Uswahilini na Joshua Fredy Laizer (23) mkazi wa Levolosi wanaendelea kupatiwa matibu katika Hospitali ya Mount Meru Arusha.
Chanzo cha ajali hiyo ni mwendokasi wa pikipiki ambazo zilikuwa zinatokea Moshi kwenda Arusha huku zikiyapita magari mengine (kuovertake) bila kuchukua tahadhari hali iliyopelekea kwenda kugongana na gari hilo.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linaendelea kutoa wito kwa madereva wote pamoja na watumiaji wa vyombo vya moto kufuata sheria za usalama barabarani ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea kutokana na ajali. Pia tutaendelea kutoa elimu na kuchukua hatua kali za kisheria kwa madereva wote wazembe ikiwemo kuwafungia leseni zao na kuwafikisha mahakamani ili hatua zaidi zichukuliwe dhidi yao.
IMETOLEWA NA:
JUSTINE MASEJO – ACP
KAMANDA WA POLISI
MKOA WA ARUSHA