NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew,akimkabidhi Tuzo ya Heshima Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule iliyotolewa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango wake katikka Tasnia ya Habari wakati wa tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) .
MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule,akizungumza wakati wa tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) lililofanyika jijini Dodoma.
MWENYEKITI wa Kamati ya Maandalizi Bi.Sakina Abdulmasoud,akielezea lengo la tamasha hilo wakati wa tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) lililofanyika jijini Dodoma.
MKURUGENZI Mtendaji wa WazoHuru Media Bw.Mathias Canal,akizungumza wakati wa tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) lililofanyika jijini Dodoma.
NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew,akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma mara baada ya kufungua tamasha la usiku wa Habari Dodoma lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Dodoma (CPC) na kuhudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe.Rosemary Senyamule,Viongozi wa Vyama vya Siasa, waandishi wa Habari wa mkoa huo na wadau mbalimbali wa sekta hiyo lililofanyika jijini Dodoma.
PICHA ZOTE NA ALEX SONNA
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KLABU ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Dodoma(CPC), imeiomba serikali kuondoa malipo ya usajili wa mitandao ya kijamii inayomilikiwa na vilabu vya waandishi wa habari kwa kuwa haiendeshwi kibiashara bali inatoa huduma za kuhabarisha jamii.
Mwenyekiti wa CPC, Mussa Yusuph ametoa ombi hilo alipokuwa akisoma risala ya klabu hiyo kwa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew kwenye hafla ya usiku wa waandishi wa habari mkoani Dodoma iliyoandaliwa na CPC kwa udhamini wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji(EWURA), Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na taasisi ya Wazo Huru.
Aidha, amesema kwa niaba ya vilabu 28 vya waandishi wa habari nchini, wanaomba serikali kutoa msamaha wa malipo ya blog za vilabu nchini kutokana na mitandao hiyo haiendeshwi kibiashara bali inatoa huduma za kuhabarisha umma.
“Blog hizi hazifanyi biashara hivyo kwa mara kadhaa tumeshindwa kulipia TCRA hivyo tunaomba zipewe msamaha ili ziendelee kuhabarisha umma,”amesema.
Aidha, amewaomba wadau kusaidia kutatua changamoto zinazowakabili ikiwamo uhaba wa vitendea kazi na ujenzi wa ofisi ili kubeba idadi kubwa ya wanachama.
“Ofisi yetu kwa sasa imekuwa ndogo hivyo kushindwa kukidhi kubeba idadi kubwa ya wanachama kwa wakati mmoja, pia tuna changamoto kubwa ya thamani za ofisi hivyo tunapata changamoto kubwa pindi waandishi wengi wanapohitaji kutumia ofisi kwa wakati mmoja.”
“Uhaba wa vitendea kazi kwa wanachama hasa kipindi ambacho Mkoa unakuwa na shughuli nyingi na kubwa kama vikao vya Bunge na mikutano ya kitaifa, vifaa hivyo ni Kamera na Kompyuta,”amesema.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri Kundo ameahidi kutembelea ofisi za klabu hiyo na kuangalia namna ya kusaidia kutatua changamoto zilizobainishwa.
“Nipongeze klabu ya Dodoma kwa hatua hii kubwa ya kuwa na blog, nipongeze pia kwa kuwa na Ofisi napenda niwahakikishie serikali itaendelea kuwa pamoja nanyi hasa ikizingatiwa serikali imehamia Dodoma, Wizara pamoja na wadau tutaendelea kutatua changamoto za sekta ya habari,”amesema.
Hata hivyo, amesema Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameendelea kuboresha mazingira ya waandishi wa habari na kuweka misingi ya kisheria ili kupata taarifa.
“Katika gharama ya usajili wa blogs Rais aliagizwa zipitiwe upya na zikapitiwa na tutaendelea kufanya mapitio ili kufikia hatua ambayo kweli itasaidia wanahabari,”amesema.