************************
Na Mwamvua Mwinyi,Chalinze
MBUNGE wa Jimbo la Chalinze ambae pia ni Naibu Waziri wa Ardhi , Ridhiwani Kikwete amewaasa wakandarasi pamoja na maeneo ambayo yanazungukwa na ujenzi wa miradi mbalimbali ya Serikali kuhakikisha inatoa kipaombele cha ajira kwa wazawa wanaozunguka miradi hiyo.
Akiwa katika muendelezo wa ziara yake kitongoji cha Magome kata ya Pera pamoja na kutembelea ujenzi wa mradi wa kituo cha kupozea umeme Chalinze alieleza, wananchi wa chalinze wanastahili pia kupata fursa ya ajira zilizopo kutokana na uwepo wa ujenzi wa Miradi hiyo.
Hata hivyo Ridhiwani alieleza, ziara ya kukagua shughuli za Maendeleo na kuzungumza na wananchi imeendelea kata ya Pera na ataendelea kwa kata na kata kujua kero za wananchi na kuzitatua na kuisemea Serikali.
Hatua kubwa kimaendelea inaendelea kupigwa na mabadiliko yanaonekana ambapo amewashukuru wana Chalinze kwa kuendelea kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na Serikali kwa mambo makubwa yanayofanyika .
Mwakilishi wa Tanesco Elieza Minja alieleza, mradi huo unaenda kumaliza changamoto kata ya Pera na maeneo mengine na kuhusu ajira za hatua ya ujenzi wapo baadhi ya wananchi waliopata ajira kwenye mradi huo.
Alieleza,ajira zitapatikana muda si mrefu ili kusaidia baadhi ya wananchi wenye mahitaji .