*********************
NA VICTOR MAKINDA
Katika kuhakikisha mazingira yanakuwa safi, kuepukana na magonjwa mbali mbali ya mlipuko, Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira mjini Igunga ( IGUWASA) wilayani Igunga Mkoani Tabora ipo katika hatua za mwisho za kuanza kuteleza mradi wa ujenzi wa mfumo wa kusafisha maji taka utakaogharimu Shilingi Bilioni 1.8.
Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa IGUWASA, Humphrey Mwiyombela, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Igunga jana kueleza hatua mbali mbali za miradi inayotekelezwa na mamlaka hiyo pamoja na mipango ya baadae ya kuendelea kuboresha huduma za maji safi na usafi wa mazingira wilayani hapa.
Mwiyombela alisema kuwa Mamlaka hiyo ipo katika hatua za mwisho za kuanza kwa mradi huo ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kuufanya mji wa Igunga kuwa wa kisasa zaidi kwani ujenzi huo utakwenda sambamba na ununuzi wa magari mawili ya maji taka.
“ Kwa sasa hatuna eneo rasmi lililoandaliwa kitaalamu kwa ajili ya kutumika kumwaga maji taka hali ambayo inahatarisha afya za wananchi. Alisema Mwiyombela..
Akizungumzia upatikanaji wa maji safi wilayani Igunga, Mwiyombela alisema kuwa IGUWASA imefikia asilimia 89 ya kusambaza huduma ya maji kwa wananchi ikiwa malengo ni kufikia matakwa ya ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 inayoagiza upatikanaji wa maji kwa asilimia 95 ifikapo mwaka 2025.
“ Katika kuhakikisha tunaongeza idadi ya watumiaji wa maji tunaende kuweka magaea kusambaza mtandao wa maji maeneo mbali mbali sambamba na kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa kutumia maji safi kwa afya zao ili waweze kutumia maji safi na kuachana na maji ya madimbwi.” Alisema.
Aliongeza kusema kuwa katika kuongeza idadi ya wananchi wanaotumia maji safi kwa kuunganishiwa mabomba, IGUWASA huwaunganishia huduma hiyo kwa mkopo ambapo hutakiwa kulipa kidogo kidogo baada ya malipo ya awali.