Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Pindi Chana akizungumza na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu na Watendaji wengine wa Wizara hiyo leo Februari 18, 2023 Kawe Dar es Salaam wakati alipofanya ziara katika eneo la Ekari 12 litakalojengwa viwanja vya michezo mbalimbali pamoja na matamasha (Sports and Arts Arena).
Na Shamimu Nyaki
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana Februari 18, 2023 amefanya ziara katika eneo litakalojengwa viwanja kwa ajili ya michezo ya ndani lililopo Kawe Dar es Salaam, ambalo litatumika katika michezo ya kuogelea, masumbwi, mpira wa netiboli, wavu pamoja na matamasha mbalimbali.
Mhe. Pindi Chana ametumia nafasi hiyo kutoa pongezi kwa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutekeleza agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutoa eneo hilo lenye ukubwa wa Ekari 12, ambapo likikamilika litakua na uwezo wa kuchukua watu takriban 16, 000 kwa wakati mmoja.
Waziri Chana amewataka Watendaji wa Wizara kuhakikisha michakato yote inayotakiwa inakamilika mapema ili ujenzi uanze na kukamilika kwa wakati.
Mhe. Dkt. Chana aliongozana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Saidi Yakubu, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Michezo Ally Mayay, Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ununuzi Bw. Masubo Masubo, Mhasibu Mkuu Bw. Deogratias Mbinga pamoja na Maafisa wengine wa wizara.