NJOMBE
Mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina la Emilio Sanga(35)mkazi wa Mtaa wa Ramadhani halmashauri ya mji wa Njombe ametelekezewa watoto wanne na mkewe ,baada ya kuugua muda mrefu na kisha kupooza nusu ya mwili wake.
Mwanaume huyo ambaye awali alikuwa akiishi nyumba ya kupanga na familia yake miezi mine baada ya kukimbiwa na mkewe aliamua kwenda kanisani mtaani hapo kuomba msaada wa hifadhi baada ya kushindwa kufanya kazi na kupata fedha ya kulipa pango sambamba na kulea watoto wake.Hujafa hujaumbika! Usemi ambao umejidhihirisha kwa bwana Emilio Sanga ambaye kwa miaka zaidi ya 10 alikuwa akiishi kwa amani na mkewe na kufanikiwa kupata watoto wane huku wakishirikiana kulea familia lakini punde tu baada ya kuugua na kupooza viungo vya mwili wake na kupoteza uwezo wa kufanya kazi ,akakimbiwa na mwenza wake.
Kwa kipindi cha miezi mine tangu akutwe na shida hiyo , amekuwa akiishi kwa shida na watoto wake kwenye nyumba ya kupanga na kisha kuamua kwenda kanisani kuomba hifadhi kwasababu hana tena uwezo wa kufanya kazi hali ambayo inamsukuma pia akiomba serikali na wadau kuona namna ya kumsaidia.
“Nilipougua na kuamua kukaa nae chini na kumueleza namna maisha mapya yatakavyokuwa katika familia kwasasa ,mke wangu alinijibu kwa hasira nikaamua kukaa kimya”alisema Emilio Sanga Roida Nyagawa mshirika wa kanisa la TAG lililompa hifadhi kwa muda mwanaume huyo anasema kipindi cha nyuma familia hiyo ilikuwa ikiishi kijijini kanisani hapo kwa amani lakini miezi michache baada ya kuugua na kupooza viungo na kupoteza uwezo wa kufanya kazi akaamua kuja kuomba hifadhi kanisani kwetu.
“Bwana Emiliano alikuja kanisani kwetu kuomba msaada wa hifadhi nasi tukampokea kwasababu alikuwa muumini wetu”alisema Roida Nyagawa muumini wa kanisa TAG Ramadhani.
Ukatili uliyofanywa na mwanamke kwa mwanaume huyu ,Unafika katika jumuiya ya Wanawake CCM mkoa-uwt inayoongozwa na Scholastica Kevela na kisha kuamua kumtembelea kumpa pole na msaada wa fedha.
Wakiwa katika eneo alilopata hifadhi mwanaume huyo aliyefanyiwa ukatili na mkewe mwenyekiti wa UWT Njombe Kevela akaonya vikali tabia iliyofanywa na mwanamke huyo aliyetelekeza watoto na mumewe baada ya kuugua na kisha kusema kwamba chama hakitamtupa mwanaume huyo katika kipindi hiki kigumu.
“Kitendo kilichofanywa na mwanamke huyu ni ukatili kwasababu ameondoka nyumbani na kuacha mumewe mgonjwa na watoto wanne ,Tunapaswa kuwa wavumilivu katika ndoa kama ambavyo maandiko yanatutaka tuwe”alisema Scholastica Kevela mwenyekiti UWT njombe
Kwa upande wake Betrice Malekela mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Njombe amesema tumezoea kuona wanaume ndiyo wanakatiliwa kwa kutelekezwa na waume zao lakini hapa Njombe Mwanamke huyu ametuchafua kwasababu yeye ndiyo ametelekeza watoto na muwe akiwa na hali mbaya kiafya hivyo sisi tutashikamana nae katika kipindi hiki kigumu.
Awali ofisa ustawi halmashauri ya mji wa Njombe Vikiana Kiwelu amesema serikali imepokea taarifa za ukatili huo na kisha kuanza kuufanyia kazi ikiwa ni pamoja na kutafuta shule za kuwarudisha shule watoto hao huku pia akisema jamii inapaswa kudhibiti ukatili wa kiuchumi uliyofanywa na mwanamke huyo.
“Tunapaswa kuupiga vita ipasavyo ukatili wa kiuchumi uliofanywa na mwamake mwenzetu huyu kwasababu unamuweka kwenye hali mbaya mwanaume na watoto”alisema Vikiana Kiwelu ofisa ustawi.