Kiasi cha shilingi milioni 516 kimetolewa na Serikali kuu kupitia mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF ili kujenga miundombinu ya Elimu katika kata ya Bugogwa wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza
Hayo yamebainishwa na Mbunge wa Jimbo la Ilemela ambae pia ni Waziri wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula wakati wa ziara yake ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya jimbo hilo ambapo amemshukuru na kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa namna anavyowajali wananchi wa Ilemela Kwa kutoa fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na iliyokwishakutekelezwa ndani ya jimbo hilo pmoja na kuwaasa wananchi kuhakikisha wanaitunza na kuilinda miundombinu hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti wizi wa vifaa vya ujenzi
‘.. Ukiiba vifaa vinavyotumika kujengea miundombinu hii hauikomoi Serikali, haumkomoi mkurugenzi zaidi na zaidi tutakuwa tunajirudisha nyuma kimaendeleo niwaombe tuwafichue wezi wanaokwmisha miradi ya maendeleo ..’ alisema
Aidha Mhe Dkt Mabula ameutaka uongozi wa kata na mtaa kuhakikisha wanawachukulia hatua kali za kisheria watu wote watakaobainika kuiba vifaa vya ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na kudhibiti vitendo hivyo visiendelee
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa wilaya ya Ilemela Ndugu Godfrey Mzava amebainisha kuwa utekelezaji wa mradi wa miundombinu ya Elimu Kwa kata ya Bugogwa unajumuisha ujenzi wa madarasa manne, jengo la utawala, ujenzi maabara mbili na bweni moja la wanafunzi lenye uwezo wa kubeba watoto themanini
Nae mratibu wa mpango wa kunusuru kaya masikini TASAF wilaya ya Ilemela Bwana Leonard Donald amefafanua kuwa utekelezaji wa mradi huo ulikabiliwa na changamoto za kiulinzi na usalama hapo awali pamoja na changamoto za kizabuni mambo ambayo yameshachukuliwa hatua Ili kuwezesha mradi huo kuendelea
Akihitimisha Mwenyekiti wa Serikali ya mtaa wa Kimanilwe-Ntemi kata ya Bugogwa Bwana Lutu Shija Mikomangwa amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hasan kwa kutoa fedha za utekelezaji wa mradi huo pamoja na kumpongeza Mbunge wa Jimbo hilo Mhe Dkt Angeline Mabula Kwa ufuatiliaji wa fedha za mradi na mkurugenzi wa manispaa ya Ilemela Mhandisi Modest Apolinary Kwa usimamizi wa mradi huo huku akiwaomba wananchi wake kuendelea kuiunga mkono Serikali katika shughuli za maendeleo