Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer amewapongeza Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) na idara ya afya kwa kuwavisha nguo.
Kiria ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye kikao cha Baraza la Madiwani, alipokuwa akitoa salamu za CCM na kuzungumza mambo mbalimbali ya maendeleo na changamoto za eneo hilo.
Amesema meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Simanjiro, mhandisi Joanes Martin na Mganga mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro (DMO) Dkt Aristidy Raphael wanastahili pongezi kwani idara za maji na afya zinafanya vyema.
“Watu wa maji na afya wametuvika nguo Simanjiro, pamoja na polisi wanaolinda usalama wa raia na mali zao, kwa kweli tunawapongeza mno kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo,” amesema Kiria.
Amesema mtaalamu lazima afikishe huduma ya jamii kwa wakati kwani baadhi ya maeneo kuna changamoto ikiwemo migogoro ya ardhi ambayo ipo Simanjiro kwa sehemu kubwa.
“Tumechoka na migogoro ya ardhi ya kata kwa kata, kijiji kwa kijiji na mtu na mtu ilihali idara ya ardhi ipo wao ni wana sayansi wenye kuhesabu kuwa moja jumlisha moja ni mbili hawadanganyi, migogoro inatoka wapi sasa?” amehoji na kuongeza;
“Idara ya ardhi wanapaswa kutoa taarifa ya mwaka mzima, migogoro inatokea wapi, tusaidiane tumalize migogoro, watendaji wa vijiji na kata badilikeni msiwe chanzo cha migogoro.”
Amesema watumishi wa idara ya ardhi ni wanasayansi hivyo wasiwe wanasiasa kwani mashamba makubwa yanaporwa na baadhi ya wahuni na wao wamenyamaza kimya bila kuchukua hatua.
“Hatuna shida na mmiliki wa ardhi ambaye amemiliki kihalali ila wajanja wachache wamechukua ardhi kihuni, mtu anamiliki ekari 2,000 za ardhi na amepata bila halali, tumepewa mamlaka tuzitumie ipasavyo,” amesema Kiria.
Amesema watumishi wanaotambulika kisheria hawachukui hatua, mtu wa maji na daktari wa wilaya wamewavika nguo na mtaalamu yeyote anapaswa kutambua kuwa akiondoka Simanjiro awe ameacha alama.
“Wewe ukiwa mtumishi unapaswa kujiuliza kuwa endapo ukiondoka kwenye wilaya ya Simanjiro utakuwa umeacha nini kitakachokufanya ukumbukwe na jamii au utaondoka tuu bila kuacha chochote?” amehoji Kiria.
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro Jacob Kimeso amempongeza Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya kwa hotuba yake na kumuasa kuwa chama kiwachukulie hatua viongozi wanaowajibika kwao.
“Wenye mamlaka ya kuchukuliwa hatua na chama wachukuliwe kwani migogoro mingi ya ardhi inatokana na viongozi wa vitongoji na vijiji na hali Simanjiro siyo nzuri tunapaswa kulinda hiki kipande kilichobaki,” amesema Kimeso.