Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana (kushoto) akipokea baadhi ya nyaraka kutoka kwa Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa (kulia) wakati wakikabishiana Ofisi za Wizara hiyo Mtumba Februari 17, 2023 jijini Dodoma.
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana na Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Mohamed Mchengerwa wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Februari 17, 2023 jijini Dodoma.
*****************************
Na Eleuteri Mangi
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Balozi Dkt. Pindi Hazara Chana amesema ataendelea kushirikiana na watendaji wa Wizara hiyo, watumishi pamoja na wadau ili iendelee kung’ara ndani na nje ya nchi kama ilivyo sasa.
Waziri Balozi Dkt. Chana amesema hayo Februari 17, 2023 katika Ofisi za Wizara hiyo Mtumba jijini Dodoma baada ya kukabidhiwa Ofisi na Waziri Mhe. Mohamed Mchengerwa ambaye amehamishiwa Wizara ya Maliasili na Utalii.
“Kipekee namshukuru sana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa imani kubwa ambayo ameendelea kutupa, tumeswichi, tunamuahidi hatutamuangusha ana matumaini makubwa na hizi Wizara zetu mbili na hata siku ya kutuapisha alisema tufanye kazi pamoja kwa kushirikiana” amesema Balozi Dkt. Chana.
Amesema kuwa, menejimenti ya Wizara inawataalamu wazuri ambao wataendelea kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Wizara hiyo na ataendedeleza mazuri yaliyofanywa na mtangulizi wake.
“Tumeambiwa pale tulipofika tuzidi kusonga mbele, uwezo tunao, sababu na nia tunayo ya kuipeleka mbele Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mimi nimeipenda slogan ya hii Wizara, kuwa ni ya furaha, amani, upendo na ni nguvu shawishi ya Serikali” amesema Waziri Balozi Dkt. Chana.
Aidha, Dkt. Chana amesema kuwa Wizara hiyo inawashirikisha vijana wengi katika sekta rasmi na isiyo rasmi katika suala la ajira kwenye sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo vijana wengi wanajiajiri na kujipatia kipato cha mtu mmoja mmoja na kuongeza Pato la Taifa (GDP).
Ameongeza kuwa ni muda mwafaka sasa wa kupeleka mbele sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambayo ni maeneo ya kufurahi lakini pia ni fursa ya kutengeneza pesa mfukoni kwa kuwa kipaji ni mtaji, taifa litanufaika na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) watapata fedha za maendeleo na kutoa huduma kwa jamii.
Akitoa neno la shukrani, Naibu Waziri Mhe. Pauline Gekul amewaahidi ushirikiano viongozi wapya Waziri Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana na Katibu Mkuu Bw. Saidi Yakubu katika kutekeleza majukumu yao ili kufanikisha malengo ya Serikali.
Naibu Waziri Gekul ametaja miongoni mwa miradi inayoendelea katika wizara hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa Kiwanja cha Michezo Dodoma, uboreshaji wa uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam, uendelezaji wa Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya pamoja na uboreshaji wa shule 56 za kuendeleza vipaji vya Michezo nchini.