Jengo la huduma ya mionzi katika Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga inayojengwa katika eneo la Kigonsera.
Jengo la maabara katika Hospitali hiyi likiwa limekamilika kwa asilimia 100.
Baadhi ya watumishi wa kitengo cha maabara Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga wakiwa kazini.
Jengo la Wagonjwa mahututi likiwa katika hatua za mwisho kukamilika.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya wilaya Mbinga George Mhina wa pili kushoto,akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wafanyakazi wa Hospitali ya Halmashauru ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma,wa tatu kusho Mganga mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt Amad Mwalukunga.
Na Muhidin Amri,
Mbinga
MRADI wa ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya wilaya Mbinga mkoani Ruvuma unaotekelezwa kwa gharama ya Sh.bilioni 1.5 umefikia asilimia 98 ya utekelezaji wake.
Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri hiyo George Mhina amesema,hadi sasa majengo matano kati ya saba ambayo ni maabara,jengo la wangonjwa wa nje(OPD),kichomea taka,jengo la mionzi,jengo la bohari ya dawa na la kufuria yamekamilika.
“katika awamu ya tatu ambayo ni ya mwisho tutajenga jengo la wodi ya wazazi ambalo ndani yake kutakuwa na huduma ya upasuaji na kulaza akina mama wanaotoka kujifungua na jengo la utawala,tuko hatua ya mwisho ya kumpata mkandarasi atakayejenga jengo hilo”amesema Mhina.
Amesema,Hospitali hiyo itakapo kamilika itahudumia zaidi ya watu 255,000 kutoka vijiji vya Halmashauri ya Mbinga na wananchi wa wilaya jirani ya Songea na Nyasa.
Hali kadhalika amesema,kwa sasa wameanza kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje,hata hivyo matarajio yao katika kipindi cha miezi mitatu ijayo,waanze kutoa huduma ya upasuaji kwa akina mama wajawazito hasa wale watakaoshindwa kujifungua kwa njia ya kawaida.
Pia amesema,mwishoni mwa mwezi huu,wataanza kutoa huduma za mionzi( X-ray) na Ultrasound kwa kuwa jengo lake limekamilika na wanachosubiri kupata vifaa kutoka bohari ya dawa nchini(MSD)yenye dhamana ya kusambaza dawa na vifaa tiba kwenye vituo vya kutoa huduma za matibabu vya serikali.
Amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kutoa fedha ambazo zinatumika katika utekelezaji wa mradi huo na miradi mingine ya maendeleo kwa Halmashauri ya Mbinga.
Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Amad Mwalukunga amesema,kuanza kwa huduma katika Hospitali hiyo kumewasaidia wananchi wa Halmashauri ya wilaya Mbinga kumaliza kero ya kwenda hadi Hospitali ya St Joseph Peramiho umbali wa kilomita 80 na Hospitali ya wilaya Mbinga iliyopo umbali wa km 20 kufuata matibabu.
Dkt Mwalukunga ametaja magonjwa yanayowasumbua wananchi wa ukanda wa Kigonsera ni malaria na hali hiyo inatokana na asilimia ni wakulima ambao wakati huu wa masika wengi wao wanaishi mashambani ambako wanakutana na changamoto ya kuumwa na mbu wanao sababisha ugonjwa huo.
Ameiomba Serikali kuitupia jicho Hospitali na kutoa fedha ambazo zitawezesha kukamilisha kabisa ujenzi wake ili wananchi waweze kupata huduma zote muhimu, badala ya kwenda maeneo mengine.
Mmoja wa wananchi aliyekutwa akipata matibabu Nassibu Mapunda,ameishukuru Halmashauri ya wilaya Mbinga kujenga Hospitali hiyo kwani licha ya kutokamilika,wameanza kupata huduma karibu na kupata muda kufanya kazi nyingine za kiuchumi.
Mapunda amesema,hapo awali walikuwa kwenye mateso makubwa ya kwenda Halmashauri nyingine kwa ajili ya kufuata matibabu, lakini sasa wanafurahi kuona baadhi ya huduma hizo zinapatikana karibu na makazi yao.
Hata hivyo,Mapunda ameiomba serikali kuwajengea barabara ya kutoka barabara kuu ya Songea-Mbinga hadi Hospitali kwa kiwango cha lami au changarawe ili kurahisisha usafiri wa kufika Hospitali.