Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Mwalimu wa Shule ya Sekondari Loiler iliyopo Mji Mdogo wa Mbalizi Mkoani Mbeya aitwaye PETER EMMANUEL [29] Pamoja na Mlinzi wa Shule hiyo aitwaye HARUNA ISSA [30] Mkazi wa Iwala kwa tuhuma za kumshambulia kwa viboko sehemu mbalimbali za mwili mwanafunzi wa Shule hiyo wa kidato cha IV aitwaye RAULENCE NICHOLOUS [16] Mkazi wa Mwangake.
Ni kwamba mapema Februari 12, 2023 huko katika Shule ya Sekondari Loiler mwalimu huyo kwa kushirikiana na mlinzi wa Shule hiyo walimtuhumu mwanafunzi RAULENCE NICHOLOUS kuiba maandazi matano ambayo kila andazi ni Tshs.300/= hivyo jumla ya maandazi yote ni Tshs. 1,500/= katika duka la shule hiyo na ndipo walimshambulia kwa viboko na kumsababishia majeraha sehemu ya paji la uso, mkono wa kushoto na magoti yote mawili.
Baada ya kumshambulia na kumjeruhi, siku hiyo ya tukio majira ya saa 05:00 usiku walimkimbiza Hospitali Teule ya Ifisi kwa ajili ya matibabu. Jeshi la Polisi kupitia wasiri wake lilipata taarifa na kufanya ufuatiliaji na kubaini kutokea kwa tukio hilo na hatimaye kuwakamata watuhumiwa wote wawili.
Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa wito kwa jamii kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani muda wowote kuanzia sasa.