MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) Arch.Daudi Kondoro,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 14,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za wakala huo katika kipindi cha mwaka 2022/23.
Na. Alex Sonna-DODOMA
WAKALA wa Majengo Tanzania (TBA) imefanikiwa kuendelea kutekeleza malengo iliyojiwekea kwenye Mpango Mkakati wake wa Mwaka 2021/22-2025/26 kwa kutoa huduma ya uhakika ya makazi kwa Serikali na watumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa leo Februari 14,2023 jijini Dodoma na Mtendaji Mkuu wa TBA Arch.Daudi Kondoro,wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za wakala huo kwa waandishi wa habari.
Arch.Kondoro,amesema kuwa wameendelea kutoa huduma ya uhakika ya makazi ya nyumba 1,622 kwa kuwapangishia watumishi wa umma na nyumba 7,757 kuwauzia watumishi wa umma Tanzania Bara.
”Tumefanikiwa kupata miradi mikubwa ya Ubunifu, Usanifu na Usimamizi wa majengo ya Serikali ambapo TBA imefanya Usanifu na Ubunifu wa Ikulu ya Chamwino, Usanifu na Ubunifu wa Mji wa Serikali awamu ya kwanza na ya pili, pamoja na miradi mingine ya Serikali nchi nzima”amesema Arch.Kondoro
Ameeleza kuwa wamefanikiwa kuhuishwa kwa Sheria iliyoanzisha TBA. Mabadiliko ya Sheria hii itaiwezesha TBA kuongeza uwezo wa kuendeleza maeneo yake katika maeneo mbalimbali hapa nchini.
Pia itatoa nafasi ya kushirikiana na Sekta Binafsi jambo litakaloongeza fursa za uwekezaji na kuweza kujenga nyumba nyingi zaidi zitakazowanufaisha watumishi wa umma na wasio watumishi wa umma.
Aidha ameongeza kuwa wamefaanikiwa kutengeneza fursa za ajira na kutoa mafunzo kwa vitendo ambapo TBA imetengeneza ajira takribani 100,000 kwa vijana wenye ujuzi na wasio na ujuzi kupitia miradi inayotekelezwa nchini.
“Utekelezaji wa Miradi Mikubwa ya Kimkakati Kitaifa, TBA tumefanya ubunifu na kujenga nyumba 644 za Makazi kwa waliokuwa wakazi wa Magomeni Kota, nyumba za makazi kwa wataalamu katika mradi wa Bwawa la kufua umeme wa Mwalimu Nyerere katika Bonde la Mto Rufiji, usimamizi katika miradi ya ujenzi wa vihenge vya kisasa na Usimamizi wa ujenzi wa rada za kuongozea ndege”, ameeleza Arch.Kondoro
Aidha amesema wameendelea kusimamia na kukarabati majengo ya Serikali ambapo mpaka sasa jumla ya nyumba na majengo 3,437 yameshakarabatiwa.
Vile vile wamefanya Udhibiti na Usimamizi Mzuri wa Rasilimali Fedha ambapo TBA inatumia mifumo iliyoandaliwa na Serikali katika kudhibiti mianya ya rushwa na kusaidia kufanya malipo kwa wakati na kwa ufanisi. Mifumo hiyo inajumuisha Mifumo ya Ulipaji Serikalini (MUSE), GePG, GRMS na manunuzi (TaNeps).
Hata hivyo amesema utumiaji wa mitambo na teknolojia ya kisasa ambapo TBA inamiliki mitambo ya kisasa inayosaidia utekelezaji wa miradi kwa ubora zaidi na kupunguza gharama za ujenzi.
Amesema kuwa Mitambo hiyo inajumuisha Mitambo ya kuchakata zege (Concrete Batching Plants), mitambo ya kushafirisha zege (Transmixers Truck), Mitambo ya uchimbaji ardhi (Excavators & Wheelloaders), mitambo ya usombaji vifaa (Dump Trucks), mitambo ya kurahisisha utendaji wa kazi (Tower crane).
Aidha Arch.Kondoro, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuiwezesha TBA kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa ikiwa ni Pamoja na kutoa fedha za ruzuku kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalim bali ya Serikali.
Pia ameongeza kuwa TBA katika kipindi cha miezi 18, umepokea jumla ya Sh. bilioni 54.2 kutoka serikalini kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya ujenzi wa nyumba za watumishi wa umma.