NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dkt.Mohammed Said Mohammed (Dimwa), akizungumza na Baraza la Wazee wa Chama Cha Mapinduzi CCM Zanzibar huko Afisini kwako Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui.
**************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar Dkt.Mohammed Said Mohammed,ameahidi kufuata ushauri,maoni na maelekezo ya wazee ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.
Ahadi hiyo ameitoa wakati akizungumza na Baraza la Wazee wa CCM Zanzibar hapo Afisini kwao Kisiwandui Unguja.
Alisema wazee ni kundi muhimu katika ustawi na uimara wa Chama Cha Mapinduzi katika kusimamia Siasa na sera zenye tija kwa wananchi.
Dkt Dimwa alieleza kuwa wazee hao ambao ni Viongozi wa zamani waliohudumu chini ya Chama Cha Afro-Shiraz Party (ASP), na wakafanikiwa kuikomboa nchi kutoka katika mikono ya utawala wa kigeni.
“Wazee wangu nakuombeni sana mnishauri na kutoa maoni yenu wakati wowote kwani naamini Chama na Serikali zake mnazijua vizuri.
Pia nakuahidi kuwa nitaumia muda,uwezo na maarifa yangu kuhakikisha Chama kinabaki salama na kila Mwanachama anajivunia kuwa katika CCM.”.Alisema Naibu Katibu Mkuu huyo.
Akizungumzia mikakati yake alisema amejipanga kusimamia kikamilifu utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 ili Wananchi wapate huduma bora za kijamii na kimaendeleo.
Aidha alisema katika kutekeleza falsafa ya kasi yenye viwango kwenye masuala ya kiutendaji atahakikisha Viongozi na Watendaji wa Chama na Serikali wanafanya kazi kwa bidii ili kufikia malengo ya kuleta Mapinduzi ya kiuchumi.
Naibu Katibu huyo, aliwambia wazee hao kuwa atasimamia miradi ya maendeleo na kubuni miradi mipya ili kuzalisha fedha zitakazotumika katika masuala uendeshaji wa Chama.
Pamoja na hayo alisema dhamira yake ni kutekeleza kwa vitendo ibara ya 5 ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2022 kuhakikisha CCM inashinda kwa kila uchaguzi wa dola .
Naye Katibu wa Baraza hilo Ndg.Waziri Mbwana,alimpongeza Naibu Katibu Dkt Dimwa pamoja na Wakuu wa Idara za Chama kwa kazi nzuri wanazofanya toka wateuliwe.
Waziri,alikiomba Chama Cha Mapinduzi kuishauri Serikali iwachukulie hatua kali za kisheria baadhi ya Watendaji na Viongozi wanao jihusisha na vitendo vya wizi wa mali za umma,rushwa,udhalilishaji wa kijinsia.
Alisema wananchi kupitia Uchaguzi Mkuu uliopita walitoa ridhaa kwa CCM kuongoza dola hivyo ni muhimu iendelee kusimamia maslahi ya watu wote bila kujali tofauti za kisiasa,kiitikadi,kidini na kikabila.