Zanzibar – Zaidi ya wacheza soka wasichana 200 watanufaika moja kwa moja kutokana na msaada wa vifaa vya michezo vyenye thamani ya Dola za Kumarekani 8,200 kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania kupitia programu yake Ruzuku Ndogo ya Diplomasia ya Umma (Public Diplomacy Small Grants Fund program).
Vifaa hivi ni sehemu ya mradi uitwao Sports4Girls (Michezo kwa Wasichana) unaotekelezwa na Asasi isiyo ya Kiserikali ya Kuwawezesha Wanawake iitwayo Women Empowerment Zanzibar (WEZA) kwa ushirikiano na Ubalozi wa Marekani Tanzania.
Mradi huu unatumia michezo kuwajengea uwezo wasichana, kuwasaidia kutimiza ndoto zao kwa kushiriki katika mazoezi ya viungo, shughuli za michezo ya kitimu, elimu ya afya na mafunzo ya stadi za maisha.
Katika hafla ya kukabidhi vifaa hivyo, wachezaji walitambuliwa kama watu wa kuigwa wanaowahamasisha wasichana wengine kuingia katika michezo huku wakikuza hadhi na kukubalika kwa wasichana katika jamii.
Afisa wa Ubalozi wa Marekani anayeshughulikia masuala ya Umma James Rodriguez aliwashukuru waandaji na washiriki kwa jitihada zao endelevu za kuboresha maisha na fursa kwa vijana wa kike wa Zanzibar.
“Michezo ni zaidi ya mazoezi ya kimwili yanayoleta manufaa katika afya yako. Michezo hufundisha stadi muhimu za maisha kama vile ushirikiano, uvumilivu na ustahimilivu, mambo ambayo yanaweza kukusaidia sana maishani na kazini.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji, na mwanzilishi mwenza wa WEZA, Bi. Petra Karume, aliishukuru Serikali ya Marekani kwa msaada na kuelezea malengo na matokeo ya mradi wa Sports4Girls.
“WEZA inatambua manufaa ya kutumia michezo kuichanganya na vipengele vingine kama nyenzo ya maendeleo.
Mradi wetu unashughulikia masuala mengi yanayowakabili watoto wa kike, kama vile kutokuwepo usawa wa kijinsia katika michezo, upatikanaji wa taarifa kuhusu afya na stadi za maisha.
Mradi wa Sports4Girls unawasaidia wasichana wa Pemba na Unguja kwa kuwapatia vifaa na mavazi ya michezo yanayoendana na kukubalika katika utamaduni wa eneo hilo, mafunzo ya stadi za maisha, sodo zinazoweza kutumiwa zaidi ya mara moja na elimu ya afya.
Warsha za afya hulenga katika usimamizi mzuri wa usafi wakati wa hedhi, lishe na utimamu wa mwili, afya ya akili na mafunzo kwa makocha wanawake kuhusu kuzingatia mbinu za ufundishaji zinazojali usawa wa kijinsia na zilizo rafiki kwa vijana zikitilia maanani mahitaji maalumu ya wasichana wanaoshiriki katika michezo Zanzibar.”
Aliongeza kuwa “Michezo na hasa michezo inayoshirikisha timu, kama vile soka, ni nyenzo yenye nguvu ya kuwajengea wasichana hali ya kujiamini, kuwajengea stadi za majadiliano, na kuimarisha sauti na ushawishi wao katika jamii. Inawajengea uwezo wa kuweka ajenda zao wenyewe, kujenga stadi mbalimbali, kutatua matatizo na kujitegemea.”
Maafisa wa serikali na watu mbalimbali wanaouunga mkono mradi huu, akiwemo refa pekee mwanamke Mzanzibari mwenye beji ya FIFA Bi. Dalila Jaffar Mtwana walihudhuria hafla hii.
Bi Dalila alisisitiza kuwa mradi wa Sports4Girls umeleta fursa sawa kwa wasichana katika michezo, kujenga ufahamu kuhusu uwezo wa wasichana na kukuza haki sawa kwa wote.
Ikiwa imeanzishwa mwaka 2020 na Bi. Petra Karume na Bi. Aisha Ali Abeid Karume, Asasi ya Women Empowerment Zanzibar (WEZA) husaidia kuwajengea uwezo wasichana na wanawake vijana kupitia michezo, elimu ya afya, elimu ya ufundi stadi pamoja na mafunzo ya stadi za Maisha. WEZA ni mbia rasmi wa mradi wa Umoja wa Mataifa uitwao United Nations Football for the Goals (FFTG).
Ilipokea fungu la kwanza la kuanzishia mradi wa Sports4Girls kutoka Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania. Warsha kuhusu afya zinazoendeshwa chini ya mradi huu huendeshwa kwa ubia na Kituo cha Afya WAJAMAMA (Zanzibar).
Aidha, Taasisi ya Kimataifa iitwayo Coaches Across Continents (CAC) inasaidia mafunzo kwa makocha wanawake kwa kutoa mtaala na msaada wa kiufundi.