************
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi TAWA Mej. Jen. (Mstaafu) Hamis Semfuko amewataka Maafisa 31 wa TAWA waliohitimu mafunzo ya kozi Na . 15 ya mabadiliko ya mfumo wa utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia kuelekea mfumo wa kijeshi kuwa chachu ya kuongeza ubunifu Ili kuongeza mapato na kuboresha utendaji kazi Kwa kuzingatia taratibu za Jeshi.
Mej. Jen. Semfuko ameyasema hayo leo Februari 11, 2023 katika hafla ya kuhitimisha mafunzo hayo yaliyofanyika katika Chuo Cha Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii Likuyu Sekamaganga kilichopo wilaya ya Namtumbo Mkoa wa Ruvuma.
“Ninataka mtambue kuwa jukumu kubwa lililopo mbele yetu ni kuhakikisha tunaboresha Uhifadhi na kuongeza mapato kutokana na Utalii unaofanyika kwenye maeneo yetu” amesema Mej. Jen. Semfuko.
“Ni matarajio ya Bodi kuwa mafunzo haya yatakuwa ni majibu sahihi Kwa kuongeza ubunifu, kukuza mapato na kuboresha utendaji kazi Kwa kuzingatia taratibu za kijeshi” amesisitiza Mwenyekiti wa Bodi ya TAWA Mej. Jen. Hamis Semfuko
Aidha Mwenyekiti huyo wa Bodi ya TAWA ameipongeza Menejimenti ya TAWA Kwa kuendesha mafunzo hayo akieleza kuwa Bodi inaamini kwamba nidhamu ya kijeshi itawezesha malengo ya Mamlaka kufikiwa Kwa haraka na itasaidia kutatua Changamoto za Usimamizi wa maeneo ya hifadhi.
Vilevile amewataka Maafisa hao kutumia weledi katika kutoa elimu kwa Jamii jinsi ya kuepuka madhara yanayotokana na Wanyamapori Wakali na Waharibifu na kuongeza matumizi ya teknolojia katika kudhibiti changamoto hizo.
Kwa Upande wake, mwakilishi wa Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi, Mlage Kabange amesema hadi Sasa jumla ya Maafisa na Askari *1,438* sawa na asilimia 77 wamehudhuria mafunzo ya “Transformation to Paramilitary” idadi ambayo inajumuisha Maafisa waliohitimu leo.
Mlage Kabange amesema Mipango ya Mamlaka ni kuhakikisha Maafisa na Askari 430 waliobaki wanapata mafunzo ya kijeshi katika Mwaka 2023/2024