MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lazaro Kilahala akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo.
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lazaro Kilahala akijibu maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari jijini Dodoma (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo.
MKURUGENZI Msaidizi Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa,akiwapongeza waandishi wa habari kwa kuendelea kutoa habari mbalimbali mara baada ya Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lazaro Kilahala kutoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na wakala huo jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Umeme na Ufundi Tanzania (TEMESA) Mhandisi Lazaro Kilahala,amesema wamesaini mikataba mitano ya ujenzi wa vivuko vipya vya Kisorya-Rugezi, Ijinga-Kahangala, Bwiro-Bukondo, Nyakarilo-Kome na Mafia-Nyamisati yenye thamani ya Sh. bilioni 33.2.
Mhandisi Kilahala ameyasema hayo jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali na majukumu yake Katika mwaka wa fedha 2022/23.
Mhandisi Kilahala,amesema kuwa hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Sh. bilioni 10.3 zilikwishalipwa kama malipo ya awali na ujenzi wa vivuko hivyo unaendelea.
“Wakala umesaini mikataba 16 ya ukarabati wa Vivuko yenye thamani Sh.bilioni 23.3 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Sh.bilioni 7.96 zilikwishalipwa na kazi zinaendelea. Aidha, ukarabati wa vivuko sita kati ya hivyo – MV. Kazi, MV. Musoma, MV. Kilambo , MV. Sabasaba, MV. TEMESA na MV. Tanga umekamilika”alisema Mhandisi Kilahala
Aidha amesema Wakala umesaini mikataba 11 ya ujenzi na ukarabati wa maegesho na miundombinu ya Vivuko yenye thamani ya Sh.bilioni 4.12 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Sh.bilioni 1.79 zilikwishalipwa na kazi zinaendelea.
Pia ameeleza kuwa Wakala umesaini mikataba mitano ya ukarabati wa Karakana na Mikataba miwili ya ujenzi wa Karakana mpya za mikoa ya Simiyu na Dodoma yenye thamani ya Sh.bilioni 7.44 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Sh.milioni 830.5 zilikwishalipwa.
“Ujenzi wa Karakana ya Simiyu umekamilika na Wakala unaendelea na taratibu za uUnunuzi ili kuanza ujenzi wa Karakana za Geita na Njombe,”amesema
Hata hivyo Mhandisi Kilahala,amesema kuwa Wakala umesaini mikataba miwili ya ununuzi na usimikaji wa mifumo ya Kielektroniki yenye thamani ya Sh.milioni 910.8 ambapo hadi kufikia mwezi Januari 2023 jumla ya Sh.milioni 435.8 zimekwishalipwa.
Amesema kwa ujumla, hadi kufikia mwezi Januari 2023 Wakala umesaini mikataba ya utekelezaji wa miradi yenye thamani ya Sh. bilioni 71.96 ambapo jumla ya Sh.bilioni 23.65 zimekwishalipwa.
“Na kati ya fedha hizo jumla ya Sh.bilioni 15.625 zimetolewa na serikali ndani ya mwaka huu wa fedha. Kiasi kilichobaki kitaendelea kulipwa kadiri utekelezaji unavyofanyika na hati za madai kuwasilishwa”amefafanua