NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Mohammed Said Mohammed,akizungumza na Wanachama wa CCM Mkoa wa Kaskazini Pemba mara baada ya kuwasili kqa ajili ya kujitambusha.
NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Mohammed Said Mohammed,akivishwa skafu mara baada ya kuwasili Mkoa wa Kaskazini “A” Pemba. VIONGOZI mbali mbali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Mohammed Said Mohammed,wakiomba dua ya pamoja katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa Rais Marehemu Dk.Omar Ali Juma katika Kijiji cha Wawi Mkoa wa Kusini Pemba. NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Mohammed Said Mohammed,akizungumza na Watendaji wakuu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kisiwani Pemba .
VIONGOZI mbali mbali wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi Dk.Mohammed Said Mohammed, wakiomba dua katika kaburi la aliyekuwa Makamu wa kwanza wa Rais wa Zanzibar Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kijijini kwao Mtambwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.
*************************
NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kimesema hakitowavumilia baadhi ya Mawaziri na Maafisa wadhamini wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao na kuisababishia Serikali hasara.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Said Mohammed ‘Dimwa’, alipokuwa akizungumza na watendaji wakuu wa serikali kwa upande wa Pemba huko katika ukumbi wa Makonyo Wawi Mkoa wa Kusini Pemba.
Alisema, Chama cha Mapinduzi kimegundua kuwa kuna baadhi ya Mawaziri na Maafisa wadhamini ndani ya serikali ya SMZ hawawezi kumsaidia Rais na kuwaonya kuwa watashauriana na mamlaka ya uteuzi ili kuangalia upya nafasi wanazotumikia.
Alifafanua kuwa kuna miradi mingi ya Serikali imeshindwa kutekelezwa kwa wakati kutokana na uzembe wa baadhi ya Watendaji na viongozi wanaoweka maslahi yao mbele kuliko maslahi ya nchi.
“Tumewapa dhamana ya kutekeleza Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025 hivyo mnaposhindwa kwenda na kasi ya Rais wa Zanzibar Dk.Mwinyi kiutendaji basi utakuwa hautufai,”alisema.
Sambamba na hayo pia Dk. Dimwa aliwaonya baadhi ya viongozi wa serikali ambao wameanza kuwabeza wananchama wa Chama Mapinduzi na kutokeleza ipasavyo maagizo ya CCM.
Alisema, wananchi katika maeneo mbalimbali wanakabiliwa na changamoto zinazoweza kuepukika kwani zingine zinatokana na uzembe wa baadhi ya watendaji wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao.
Pamoja na hayo alieleza kuwa viongozi na watendaji wa serikali wanatakiwa kutoa ushirikiano kwa wananchi wote ili kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa umma.
Hivyo alisema, hatopenda kwenda kwenye taasisi fulani na kuona mtu hana ilani ya Chama na hajui ni kwa kiasi gani ameitekeleza ilani hiyo.
Alisema, ana matumaini kuwa watendaji na viongozi wa serikali katika sekta mbali mbali wana uwezo wa kutekeleza maelekezo ya Chama.
Aidha Dimwa alisema, kiongozi yeyote aliye nyuma yake basi anatakiwa kuwa bega kwa bega na yeye katika kukitetea Chama cha Mapinduzi sambamba na kuwalinda, kuwatetea na kuwasemea Marais Dk. Samia na Dk. Mwinyi.
Kupitia ziara hiyo Naibu Katibu Mkuu huyo Dkt.Dimwa, akiwa ameongozana na Sekretarieti yake, walizuru makaburi ya viongozi wa Kitaifa ambao ni aliyekuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk.Omar Ali Juma na aliyekuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Seif Sharif Hamad kisiwani Pemba.