Waziri wa Kilimo Mheshimiwa Hussein Bashe alipotembelea na kukagua ghala la kuhifadhia mbolea ya ruzuku eneo la SAMCU mjini Songea ambapo pia alitoa maagizo ya kuongeza vituo vinne vya kusambazia ,mbolea katika Halmashauri ya wilaya ya Songea hali ambayo imesaidia kuwasogezea wananchi mbolea hivyo kupunguza gharama na usumbufu wa kufuatilia mbolea mjini Songea
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas ambaye amekuwa akifanya ziara za kikazi kutembelea wilaya zote vijijini na kuzungumza na wakulima na kusikiliza changamoto zao kwenye mbolea ya ruzuku na kuzitatua
Shamba la mahindi katika kijiji cha Lipokela Halmashauri ya wilayan ya Songea ambalo limezalishwa mahindi msimu huu na kuwekwa mbolea ya ruzuku hali ambayo inamhakikishia mkulima mapato makubwa
Mbolea ya ruzuku ikiwa imehifadhiwa katika moja ya maghala ya kuhifadhia mbolea ya ruzuku mjini Songea
……………………………….
Baadhi ya wananchi Wilayani Songea mkoani Ruvuma wamepongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa mbolea ya ruzuku ambayo imewawezesha wananchi wengi kununua na kuongeza uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Malieta Komba Mkazi wa kijiji cha Mwanamonga Songea vijijini amesema mbolea ya ruzuku kuuzwa kati ya shilingi 50,000 hadi 70,000 kutegemea na aina ya mbolea hivyo kutoa fursa kwa wakulima wengi msimu huu kulima ambapo amesema uzalishaji unaweza kuongeza mara dufu.
Amesema katika msimu uliopita bei ya mbolea mkoani Ruvuma ilikuwa juu kati ya shilingi 100,000 hadi 150,000 hali ikiyosabibisha wakulima masikini kushindwa kununua hivyo kuathiri uzalishaji.
Kwa upande wake Afisa Kilimo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Onesmo Ngao amesema hadi sasa katika Mkoa wa Ruvuma zaidi ya tani 56,000 za mbolea ya ruzuku zimesambazwa kwa wakulima.
Hata hivyo amesema lengo la Mkoa kwa msimu huu ilikuwa ni kusambaza mbolea ya ruzuku tani 50,000 hivyo Mkoa umevuka lengo kwa zaidi ya asilimia 100.
“Bado usambazaji mbolea unaendelea tunatarajia hadi msimu kumalizika usambazaji unaweza kufikia zaidi ya asilimia 67”,alisema Ngao.
Kwa miaka minne mfululizo Mkoa wa Ruvuma umekuwa unaongoza katika uzalishaji wa mazao ya chakula nchini na kuwa kapu la Taifa la chakula.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma