Na Mwandishi wetu, Simanjiro
MWENYEKITI wa CCM Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Kiria Ormemei Laizer amesema wananchi wa eneo hilo hawana haja na wawekezaji wahuni na waongo.
Kiria ameyasema hayo wakati akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 46 ya kuzaliwa CCM ambayo kiwilaya yamefanyika kwenye kitongoji cha Kidomunge Kata ya Naberera.
Amesema hawahitaji wawekezaji wahuni kwenye sekta mbalimbali za mifugo, kilimo, madini na maeneo mengine kwani lengo lao ni kushirikiana na wawekezaji waminifu.
“Tunawapenda wawekezaji na tunawakaribisha Simanjiro wawekeze na wawe wakweli na tutashirikiana nao ila wawekezaji wahuni na wadanganyifu hatuwataki,” amesema Kiria.
Amesema kumekuwepo na baadhi ya wawekezaji wachache wanaowekeza kwenye kilimo ambao wanashirikiana na wenyeviti wasiowaaminifu kufuja ardhi ya wananchi.
“Unakuta kuna mwekezaji amepata ardhi kiasi cha ekari 3,000 akiwa na nyaraka zisizo halali na wananchi hawana taarifa yoyote zaidi ya Mwenyekiti wa kijiji na baadhi ya wajumbe, huyo hatumtaki,” amesema Kiria.
Diwani wa Kata ya Ngorika Albert Msole amesema baadhi ya wenyeviti wa vijiji wasio waaminifu na wanaofuja ardhi wameanza kumchukia Mwenyekiti wa CCM wa wilaya kutokana na kupinga uuzaji holela wa ardhi.
“Mwenyekiti tupo pamoja na wewe kwenye hilo, endelea kusimamia na kulipinga kwa nguvu zote nasi tutapiga kelele pamoja na wewe kupinga uuzwaji ardhi holela,” amesema Msole.
Mwenyekiti wa CCM Kata ya Terrat, Soipey Koromo amesema watakuwa sambamba na Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya katika kutetea ardhi ya wananchi wa Simanjiro isiuzwe.
“Sisi ndiyo tunaishi Simanjiro na tunaifahamu Wilaya yetu, hivyo Mwenyekiti tunakuunga mkono katika kuhakikisha kuwa tupo pamoja kutetea ardhi yetu,” amesema Koromo.