Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kitelea kata ya Kilimani Halmashauri ya Mji Mbinga mkoani Ruvuma wakishiriki shughuli za ujenzi wa mradi wa zahanati iliyojengwa kwa ushirikiano kati ya wananchi na serikali kupitia Halmashauri ya Mji Mbinga.
Muonekano wa zahanati wa kijiji cha Kitelea Halmashauri ya Mji Mbinga,ikiwa katika hatua ya mwisho kukamilika.
…..
Na Muhidin Amri
Mbinga
WANANCHI wa kijiji cha Kitelea kata ya Kilimani Halmashauri ya mji Mbinga mkoani Ruvuma,kwa kushirikiana na serikali wamefanikiwa kujenga zahanati ili kuwawezesha kupata huduma ya matibabu karibu na makazi yao.
Kukamilika kwa ujenzi wa zahanati hiyo kutawaondolea kero ya kwenda hadi Mbinga mjini umbali wa km 8 kufuata huduma na zaidi ya wananchi 2,000 wa kijiji hicho watanufaika na huduma zitakazotolewa katika zahanati hiyo na hata kupata muda mwingi wa kufanya shughuli za maendeleo badala ya kufuata matibabu maeneo mengine ya mji wa Mbinga.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kuhusiana na ujenzi wa zahanati hiyo wananchi hao wamesema,wanajivua kuwa sehemu ya watu waliofanikisha ujenzi wa mradi huo muhimu kupitia fedha walizochanga na nguvu kazi walizotoa kwa kufanya kazi ndogo ndogo ikiwamo kusomba mchanga,kufyatua tofali, kuchota maji na kuchangia mbao.
Fidelius Nombo amesema,kijiji hicho hakijawahi kuwa na huduma yoyote ya afya tangu kilipoanzishwa,hivyo kujengwa kwa zahanati hiyo ni jambo Historia kwao kwa kizazi cha sasa na cha baadaye.
Nombo ameishukuru serikali kupitia Halmashauri ya mji Mbinga kwa kuwaunga mkono katika ujenzi wa zahanati hiyo ambayo imekamilika kwa asilimia 98 na sasa wanasubiria kuona huduma za matibabu zikianza kutolewa.
Aidha amesema,kwa kuwa ujenzi huo umekamilika ni vyema serikali ikaanza maandalizi ya awali kwa kupeleka vifaa na watumishi ili wananchi waanze kupata matibabu,badala ya kuendelea na mateso ya kutembea hadi Hospitali ya wilaya Mbuyula kufuata matibabu.
Gaudencia Sangana,ameushukuru uongozi wa Halmashauri ya mji Mbinga wakiongozwa na Mkurugenzi wake Grace Quintine kwa kutambua na kuunga mkono juhudi za wananchi ambapo Halmashauri imechangia kiasi cha Sh.milioni 50 zilizosaidia kufanikisha ujenzi wa zahanati hiyo.
Hata hivyo,amieomba serikali kuharakisha mchakato wa kupeleka watumishi katika zahanati hiyo ili kutoa huduma na kuwapunguzia wananchi muda mwingi wanaotumia kwenda kupata matibabu katika maeneo mengine.
Mwenyekiti wa kijiji cha Kitelea Festo Nchimbi amesema, zahanati hiyo ilianza kujengwa tangu mwaka 2019 lakini walishindwa kukamilisha kutokana na kukosa fedha na vifaa vya viwandani.
Nchimbi,amemshukuru Mbunge wa viti maalum mkoa wa Ruvuma Jackline Msongozi aliyetoa bati 50 ambazo zimetumika kufunga linta na kuwaomba wadau wengine kusaidia vifaa ili kukamilisha ujenzi huo.
Ametaja,vijiji vingine vitakavyonufaika ni Sepukila,Kilimani,Mhekela na kuiomba serikali kufungua zahanati hiyo haraka ili iweze kutoa huduma kwa wananchi.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya mji Mbinga Dkt Maximo Magehema amesema,zahanati hiyo ilianza kujengwa kwa nguvu za wananchi ambao walichangia nguvu zao zenye thamani ya Sh.milioni 41 na serikali kupitia Halmashauri ya mji Mbinga imetoa Sh.milioni 50.
Magehema ametaja kazi zilizobaki katika ujenzi huo ni kupata rangi,kuweka malumalu sehemu ya vyoo,kufunga baadhi ya milango na kufunga madirisha.