*****************
MBUNGE wa Mufindi Kusini David Kihenzile ameshinda kwa kishindo kwa mara ya pili kuongoza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo Kihenzile ameibuka kidedea baada ya kupata kura 14 sawa na asilimia 88 na kumbwaga mpinzani wake Dk Christina Ishengoma aliyepata kura 2 sawa na asilimia 12.
Kufuatia ushindi huo, Kihenzile ataongoza tena kamati hiyo kwa awamu ya pili ambayo itamalizika Julai 2025 Bunge litakapovunjwa, kujiandaa na uchaguzi mkuu wa nchi.
Awamu ya kwanza alishinda Novemba 2020 na kuiongoza kamati hiyo kwa kipindi cha miaka miwili na nusu kabla ya kumaliza muda wake jana Januari 9, 2023.
Akizungumza mara baada ya matokeo hayo, Kihenzile amesema “nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kuendelea kuniamini na kunichagua tena kuiongoza kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, naamini tutaendelea kushirikiana katika kutekeleza majukumu ya kamati yaliyo mbele yetu.”
Aidha, katika uchaguzi huo, nafasi ya Makamu Mwenyekiti ameshinda Mbunge wa Wanawake kupitia Mkoa wa Dodoma, Mariam Ditopile aliyepata kura 9 sawa na asilimia 56 akimshinda Samwel Hayuma aliyepata kura nne na Isac Francis aliyepata kura tatu.