KATIKATI ni Chifu wa Tano wa Kabila la wangoni Nduna Imanuel Zulu Mbano akiwa ndani ya Makumbusho ya Taifa ya Majimaji mjini Songea
Jemedari wa Kabila la wangoni Nduna Songea Mbano ambaye jina lake limepewa mji wa Songea,picha hiyo alipigwa na wajerumani mwaka 1906 muda mfupi kabla ya kunyongwa na wajerumani
MASHUJAA 67 wa vita ya Majimaji ambao walinyongwa na wajerumani mwaka 1906 kisha kuzikwa ndani ya makumbuisho ya Taifa ya Majimaji ambako kuna makaburi mawili,kaburi kubwa ni la mashujaa 66 ambao wamezikwa pamoja na kaburi moja ni la Jemedari wa wangoni Nduna Songea Mbano
MNARA ambao umejengwa katika eneo la Songea Club mahali ambapo walinyongwa kikatili na wajerumani mashujaa 67 mwaka 1906 kisha kwentda kuzikwa ndani ya makumbusho ya Majimaji Mahenge Songea
Baadhi ya majengo ndani ya makumbusho ya Taifa ya Majimaji
MUONEKANO wa mji wa Songea mwaka 1897
……………………………..
MJI wa Songea uliopo katika Mkoa wa Ruvuma ni miongoni mwa maeneo machache hapa nchini ambayo yana hazina kubwa ya utajiri wa kihistoria na kishujaa.
Mashujaa kutoka katika Mji wa Songea waliendeleza mapambano dhidi ya ukoloni wa Kijerumani hivyo kuchangia kikamilifu harakati za ukombozi kabla ya kupata uhuru wa Tanganyika mwaka 1961.
Jina la Mji wa Songea ni kumbukumbu ya Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na Ikulu yake katika Mji wa Songea. Mji wa Songea una majengo ya kumbukumbu za kihistoria mbalimbali yakiwemo makanisa yenye miaka zaidi ya 100.
Mhifadhi Kiongozi wa Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Bartazar Nyamusya anasema historia inaonesha kuwa Mji wa Songea ulianzishwa mwaka 1897 kama kituo cha kijeshi cha Kijerumani.
Hata hivyo anasema Mji wa Songea uliendelea kukua na kuwa Makao makuu ya utawala wa Wajerumani katika Wilaya ya Songe ana kwamba Mji huo ulizinduliwa rasmi kuwa mji wa kihistoria, kishujaa na kiutalii mwaka 2010.
Historia inaonesha kuwa Mji wa Songea uliathirika na Vita ya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907 na Vita kuu ya pili ya Dunia kati ya mwaka 1939 hadi 1945.
Licha ya Mji huo kuathirika na vita hivyo,Nyamusya anasema mji uliendelea kuwa Makao makuu ya Mkoa wa Ruvuma wakati wa utawala wa Waingereza katika Tanganyika, baada ya uhuru hadi leo bado Songea ndiyo Makao Makuu ya Mkoa wa Ruvuma.
Mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa wa Vita ya Majimaji ambapo mashujaa 67 walinyongwa mwaka 1906 kati yao mashujaa 66 walizikwa katika kaburi moja.
Nduna Songea Mbano ambaye alikuwa na umaarufu, alinyongwa na kuzikwa katika kaburi lake ambapo makaburi yote yapo katika Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Mashujaa hao 67 walinyongwa katika eneo lililojengwa Mnara wa Mashujaa wa vita ya Majimaji nyuma ya ukumbi wa Songea ambalo ni kivutio cha aina yake cha utalii katika Mji wa Songea.
Mkoa wa Ruvuma pia ulitoa mashujaa walioshiriki katika Vita kuu ya pili ya Dunia ambapo mashujaa 270 walishiriki katika vita hiyo kati yao mashujaa watatu walikuwa ni wanawake.
Makumbusho ya Majimaji yalianzishwa rasmi mwaka 1980 na kusimamiwa na Hayati Dk.Lawrence Gama wakati huo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma.
Mchakato wa kuyakabidhi Makumbusho hayo chini ya Shirika la Makumbusho ya Taifa ulianza Mei hadi Novemba 2009 ukisimamiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dk.Christine Ishengoma.
Makumbusho hayo yalikabidhiwa katika Shirika la Makumbusho ya Taifa chini ya sheria ya makumbusho ya Taifa la Tanzania, namba saba ya mwaka 1980 hivyo makumbusho hayo yalipandishwa hadhi na kuwa Makumbusho ya Taifa mwaka 2010.
Haya ni Makumbusho pekee nchini ambayo imebahatika kuwa na vifaa muhimu katika historia ya Mtanzania, mchakato uliopo hivi sasa ni Makumbusho hayo kuchukuliwa kuwa ya Kitaifa chini ya Wizara ya Maliasili na Utalii ili iwe endelevu.
Mji wa Songea ni miongoni mwa miji michache ambayo ilitoa upinzani mkali katika vita vya Majimaji ambapo katika Makumbusho hayo kuna ushahidi ambao unaonesha moja kwa moja kuwa wazee wa Songea walishiriki kikamilifu katika vita hiyo.
Makumbusho haya yaliitwa Makumbusho ya Mashujaa wa vita ya Majimaji kwa sababu ni eneo ambalo lina makaburi mawili ya mashujaa walionyongwa wakati wa vita ya Majimaji kipindi cha utawala wa Mjerumani.
Ukitazama nje ya Makumbusho hayo kuna sanamu za wapiganaji wa vita ya Majimaji.Majina ya sanamu za wapigaji hao ambao waliwahi kutawala Songea ni Mpambalyoto Soko bin Msarawani na Nduna Songea Mbano bin Luwafu.
Majina mengine ni Nduna Chabruma Gama bin Hawayi, Zimamoto Gama bin Fusi, Nkosi Mputa Gama bin Gwazerepasi, Nduna Zamchaya Gama bin Gwazerepasi, Mtepa Ntara bin Kanyoka na Nduna Usangira Gama bin Mheshimiwa Waarule.
Wapiganaji wengine ni Magodi Mbano bin Mbamba, Njorosa Mbano bin Mbamba, Masese Parangu Mbano bin Songea, Nyunyusea Mbano bin Njenje na Njorosa Mbano bin MbambaUrithi huu wa utamaduni uliopo katika Makumbusho ya Taifa.
Majimaji ni hazina kubwa ya vivutio vya utalii wa kihistoria na kiutamaduni ambaoiendelezwa unaweza kuingiza pato kwa wakazi wa Mkoa wa Ruvuma.
Makumbusho ya Taifa ya Majimaji yana malikale ambazo zimehifadhiwa na zinaweza kutumika kama kivutio cha utalii na kujifunza historia ya mashujaa na urithi ambao unapatikana katika Mkoa wa Ruvuma.
Tanzania ina nyumba kadhaa za Makumbusho ya Taifa katika maeneo mbalimbali nchini ambazo Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni Dar es salaam, Kijiji cha Makumbusho ya Taifa Dar es Salaam, Makumbusho ya Elimu Viumbe Arusha, Makumbusho ya Azimio la Arusha, Makumbusho ya Mwalimu Julius Nyerere Butiama na Makumbusho ya Taifa ya Majimaji Songea.
Imeandikwa na Albano Midelo wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma