Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi nakala za Nyaraka za Usimamizi wa Maafa, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula baada ya kuzindua nyaraka hizo kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose, Senyamule. (OPicha na Ofisi ya Wziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Nyaraka za Usimamizi wa Maafa kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na Skauti baada ya kuzindua Nyaraka za Usimamizi wa Maafa kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma, Februari 9, 2023. Kushoto kwake ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt. Angelina Mabula na kulia kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rose, Senyamule. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
*************************
*Asisitiza wanaohusika na usimamizi wa maafa watekeleze majukumu yao ipasavyo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezitaka sekta zote zinazohusika na utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa, idara au taasisi zenye jukumu la kisheria la kutekeleza kazi hiyo zihakikishe zinawajibika kikamilifu katika kushughulikia vizuri pindi maafa yanapotokea.
Amesema pamoja na uwepo wa sera na sheria ya usimamizi wa maafa na nyaraka alizozindua ambazo zimelenga kuimarisha mifumo ya uwajibikaji kwa kila sekta, ushirikiano unahitaji katika kutekeleza afua za ustahimilivu na kuzuia maafa.
Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Februari 9, 2023) wakati akizindua nyaraka za usimamizi wa maafa katika Ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma. Nyaraka zilizozinduliwa ni Mpango wa Taifa wa Kujiandaa na kukabiliana na Maafa (2022).
Nyaraka nyingine ni Mkakati wa Taifa wa Mawasiliano Wakati wa Maafa (2022), Mpango Mkakati wa Taifa wa Afya Moja (2022-2027), Mkakati wa Taifa wa Usimamizi wa Maafa (2022-2027) na Mwongozo wa Taifa wa Kupambana na Vitendo vya Kihalifu katika Bahari na Maziwa Makuu (2022).
Amesema miongozo na mipango hiyo ya usimamizi wa maafa inatoa jukumu kwa wizara, Serikali za Mitaa, hivyo taasisi pamoja na wadau wengine kuandaa mipango kazi na taratibu za usimamizi wa maafa pamoja na namna ya kushughulikia dharura pindi inapojitokeza.
Waziri Mkuu amesema nchi bado inao uwezo wa kudhibiti majanga yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu, hivyo wahusika wawajibike katika kuelimisha umma wa Watanzania namna ya kukabiliana na majanga na kusimamia kikamilifu utekelezaji wa nyaraka hizo.
“Nitoe rai kwa Watanzania wenzangu, tuwe sehemu ya watendaji wakati wa dharura zinapojitokeza badala ya kusubiri tuanze kulaumu. Wale wenye nguvu na uwezo wa kusaidia wajitokeze kuunga mkono jitihada za Serikali badala ya kuwa watazamaji mfano ilipotokea ajali ya ndege wananchi walijitokezakusaidia.”
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali kwa upande wake itaendelea kuimarisha mbinu na mikakati ya makusudi ya udhibiti wa athari zitokanazo na maafa pamoja na usimamizi wa utekelezaji wa sera, sharia na mikakati ya usimamizi wa maafa.
Pia, Waziri Mkuu amezielekeza wizara, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa na taasisi nyingine zitenge fedha kwa ajili ya kutekeleza shughuli za usimamizi wa maafa katika maeneo yao. “Waheshimiwa Mawaziri mliopo hapa, Makatibu Wakuu, Makatibu Tawala wa mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri za wilaya nendeni mkasimamie kikamilifu bajeti katika maeneo yenu ili kuwezesha usimamizi wa maafa.”
Waziri Mkuu amesema viongozi hao wanatakiwa watenge rasilimali kabla ya kutokea kwa maafa na kwa kufanya hivyo watakuwa wamejijengea uwezo wa kukabiliana na maafa hayo, pia sekta zote zilizopewa majukumu ya kusimamia maafa zihakikishe zinaratibu upatikanaji wa msaada wa kitaalamu na vifaa vya utafutaji na uokoaji.
Kwa upande wake, Muwakili Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) Bi Veronica ameihakikishia Serikali kuwa UNDP pamoja na wadau wengine wa maendeleo wataendelea kushirikiana na Tanzania katika kukabiliana na maafa.
Amesema nyaraka hizo zilizozinduliwa leo zitasaidia katika upatikanaji wa taarifa za maafa kwa wakati na hivyo kuwawezesha wahusika kuchukua hatua haraka.