MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Watumishi Housing Investments, Dk. Fred Msemwa, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 9,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali pamoja na mipango ya badaye ya shirika hilo.
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Watumishi Housing Investments, Dk. Fred Msemwa,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari leo Februari 9,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali pamoja na mipango ya badaye ya shirika hilo.
………………………………
Na.Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mtendaji wa Shirika la Watumishi Housing Investments, Dk. Fred Msemwa, amesema mahitaji ya nyumba nchini ni milioni tatu huku mkoa wa Dar es saalam pekee yake ni nyumba 400,000.
Hayo ameyasema leo Februari 9,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali pamoja na mipango ya badaye ya shirika hilo.
Dk.Msemwa amesema kutokana na mahitaji ya nyumba yaliyopo nchini shirika hilo limekuwa likijikita zaidi katika ujenzi wa nyumba za gharama nafu kwa ajili ya makundi yote nchini.
“Takwimu zinaonyesha kuwa kati ya Watanzania 100 ni 15 pekee ndiyo wenye uwezo wa kununua nyumba ya bei ya kuanzia milioni 25 na kuendelea hivyo kutokana na hali hiyo sisi tumeamua kuwa na miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu kwa ajili ya watu wote”alisema
Aidha amesema kutokana na umuhimu wa nyumba shirika hilo limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya nyumba za gharama nafu katika mikoa mbalimbali nchini.
Amesema kuwa kupitia Mfuko wa Faida fund ambao unatumia mfumo wa malipo ya Serikali wamevuka lengo kwa kukusanya michango ya Sh. bilion 12 .9 katika mauzo ya awali huku matarajio yalikuwa ni kukusanya Sh.bilioni 7 ikiwa ni ndani ya miezi miwili tangu kuanzishwa kwake.
“Hapa nchini watanzania 800,000 ndio wanaoshiriki katika uwekezaji wa pamoja wa soko la fedha, hivyo nawashauri watanzania kujitokeza kujiunga na mfuko huo ambao utawawezesha kufikia malengo, kujiletea maendeleo na kujikwamua kiuchumi,”amesema Dkt.Msemwa
Amefafanua kuwa makusanyo hayo ya Mfuko ni katika kipindi cha Novemba mwaka jana mpaka kufikia Februari 9 walikuwa na Sh.bilioni 14, na kwamba fedha hizo wameziwekeza katika masoko ya fedha ikiwemo mabenki na Serikali ambapo watanzania zaidi ya 4000 wamejiunga.
Kuhusu uendeshaji wa Mfuko huo, amesema Faida Fund unafanya kazi kwa njia ya kuuza vipande, ambapo bei ya kipande ilikuwa sh 100, mpaka sasa thamani ya kipande imefikia sh 101.1, hivyo thamani ya vipande imeendelea kukua.
Dk.Msemwa amesema, Watumishi Housing ndio wanaonunua vipande kutoka kwa wawekezaji ambao ni wanachama wa Mfuko huo watakaokuwa na uhitaji wa kuuza vipande vyao ili wapate Fedha.
Dkt. Msemwa ametaja faida ya kuwekeza kwenye Mfuko, kuwa ni pamoja na kuwa na uwezo wa kuwekeza katika masoko ya Fedha bila kulazimika kufuata mlolongo mrefu ikiwemo kwenda kwa madalali, uwekezaji hufanyika kwa njia ya simu hivyo kuokoa muda na kuwa na usalama wa fedha na kupata unafuu na kuwekeza bila tozo huku uwekezaji wako ukitambulika kwa Kasi kikubwa.
Pia amesema uwekezaji unaweza ukautumia kama dhamana pale utakapohitaji mkopo wa Benki ili kujiongeza zaidi kiuchumi na Mfuko wa faida fund ni endelevu na unalengwa sekta zote.
Kuhusu ujenzi wa nyumba amesema Nyumba 983 tayari zimejengwa kupitia taasisi hiyo ya Watumishi Houseng nchi nzima na kwamba katika ujenzi wa kila nyumba 100 Watumishi Housing huzalisha ajira kwa watu 120 hapa nchini