KAIMU Mkuu wa chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dk. Tumaini Gurumo,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 9,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chuo hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 1978.
……………………………….
Na.Alex Sonna-DODOMA
KAIMU Mkuu wa chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Dk. Tumaini Gurumo, amesema chuo hicho kinampango wa kuboresha karakana ya mafunzo kuwa ya kisasa zaidi ili kuendana na mabadaliko ya Sayansi na Teknolojia pamoja na soko la ajira.
Hayo ameyasema leo Februari 9,2023 jijini Dodoma wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za chuo hicho toka kuanzishwa kwake mwaka 1978.
”Malengo yetu ni kuboresha karakana ili kuendana na mabadiliko ya kitekinolojia ili wahitimu wanapomaliza wasipate shida wanapoingia katika soko la ajira.”amesema Dk.Gurumo
Pia,tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kukipatia chuo hichi kiasi cha Sh.bilioni 6.5 ambazo wamezitumia kwa ajili ya kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia.
“Vile vile, tunaishukuru serikali kwa kutupatia maeneo ambayo tunakwenda kujenga matawi ya chuo chetu na kusogeza huduma yetu karibu na jamii lakini pia kutokana na umuhimu wa fani hii serikali imekuwa ikitoa mikipo kwa ajili ya wanafunzi na katika mwaka huu wa masomo jumla ya wanafunzi 1,705 wamenufaika”amesema
Aidha amesema kuwa malengo ya chuo hicho ni kuanza kujenga vyombo vya usafiri wa bahari vidogo kupitia ujuzi walionao na kuviuza ili kuendelea kukuza uchumi wa bluu.
“Kujenga chuo katika ngazi ya juu ili kulingana na ukubwa wa jina tulionao na tunatarajia kujenga chuo hicho kikubwa katika ufukwe wa bahari Dar es saalam na matawi yake yatakuwa mikoani”amesema
Hata hivyo Dk.Gurumo amewataka vijana nchini kujiunga na Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) ili kunufaika na fursa nyingi zilizopo ndani na nje ya nchi katika fani za Ubahiria.