Meneja Mradi Tiketi Mtandao kutoka Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) Tadei Mwita akizungumza kwenye Semina iliyowakutanisha Wanachama wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) iliyofanyika katika ukumbi wa Mikutano uliopo kwenye Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza
Katibu tawala msaidizi Seksheni ya uchumi na uzalishaji Mkoa wa Mwanza Emili Kasagara akizungumza kwenye Semina ya Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) ambapo amewataka wajiunge kwenye mfumo wa tiketi mtandao utakaowasaidia kufanya kazi zao kwa uharaka
Wanachama wa TABOA wakiendelea kupewa semina juu ya umuhimu wa kujiunga na kutumia mfumo wa tiketi mtandao
Baadhi ya Wanachama wa Chama Cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) wakiwa ukumbini
*********************************
Na Hellen Mtereko, Mwanza
Katibu Tawala Msaidizi Seksheni ya Uchumi na Uzalishaji Mkoani Mwanza Bw. Emil Kasagara amewataka wasafirishaji wa mabasi ya masafa marefu kujiunga na kutumia mfumo wa Tiketi Mtandao na kuunganisha mifumo yao kwenye Mfumo wa Usimamizi wa Mashine za Risiti za Kielektroni (EFDMS) ili mifumo hiyo iweze kubadilishana taarifa.
Ameyasema hayo leo Jumatano Feburuari 8,2023 kwenye semina ya wanachama wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (TABOA) iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Bw. Kasagara amesema kuwa, Mfumo huo unaiwezesha Serikali kupata takwimu sahihi za uendeshaji wa Sekta ya usafirishaji nchini pamoja na kufanya maamuzi mbalimbali kwa usahihi na pia unasaidia kupunguza upotevu wa mapato kwa wamiliki kwa kuwa wanapata fedha zao pindi abiria anapokata tiketi yake.
“Mfumo huu ni mahususi kwa ajili ya usafiri wa abiria, unaruhusu mtu yeyote kukata tiketi bila ya kwenda stendi au kwenye ofisi ya basi husika, hii ni faida kwa wasafiri maana inaokoa muda na inawasaidia kupunguza adha wakati wa ukataji wa tiketI,” ameeleza Kasagara
Aidha, amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha na kuimarisha utendaji wake kwa njia ya mifumo ambayo imeongeza tija na maendeleo ya nchi kwa jumla.
Naye Meneja Mradi wa Tiketi Mtandao LATRA CPA Tadei Mwita amewasihi wasafirishaji kuzingatia Kanuni za Leseni za Usafirishaji – Mabasi ya Abiria za mwaka 2020 kwa kuwa ndizo zinazowaongoza katika utoaji wa huduma za usafirishaji nchini.
“Kanuni ya 22(j) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria kutoa tiketi kwa kutumia mfumo wa tiketi wa Kielektroni ulioidhinishwa na LATRA na Kanuni ya 23(b) na 24(d) inamtaka mwenye leseni ya kusafirisha abiria ahakikishe tiketi ya kielektroni inatolewa kwa kila abiria,” ameeleza CPA Mwita.
Ameongeza kuwa, Kanuni ya 30 inamtaka mtoa huduma ya usafiri wa abiria kutotoza nauli inayozidi kiwango kilichoidhinishwa kwa daraja husika la gari na Kanuni ya 32(1)(b) Mtoa huduma ya usafiri wa abiria ahakikishe wafanyakazi wa ndani ya gari wanapewa vifaa vya kuwawezesha kutoa tiketi za kielektroni.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Meneja TRA Mkoa wa Mwanza Bi. Millicent Igogo amesema TRA na LATRA wataendelea kushirikiana ili kuhakikisha kuwa wasafirishaji wanapata elimu na wanatumia Mfumo wa Tiketi Mtandao kwa kuwa umekuwa na tija kwa Serikali, Wamiliki na Wananchi kwa jumla katika kukuza uchumi.