HALMASHAURI ya wilaya ya Ikungi Mkoani Singida imetoa mkopo wenye thamani ya Shilingi Milioni 141 na vyerehani vitatu kutoka kwenye asilimia 10 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana,wanawake na watu wenye ulemavu.
Hatua hiyo ni utekelezaji wa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuhakikisha wanatekeleza takwa hilo la kisheria.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Justice Kijazi akizungumza na mtandao huu Februari 7,2023,amesema huo ni muendelezo wa utoaji wa mikopo kwa makundi ili kuyawezesha kiuchumi na hivyo kupunguza umaskini na utegemezi.
Vikundi vilivyopewa mikopo hiyo ni Jonelaa Siuyu,Ushirika Siuyu,Be the light mbumbuiko,Vijana chapakazi Ikungi,Heshima wanawake Ikungi,Kwaja matongo walemavu,Igembe isabo ngongosoro,Ipililo ngongosoro,Kidundu vijana kipunda,Mshikamano iyumbu,Tumaini stars iyumbu,Rohosafi vijana iyumbu na Faraja wanawake Mgungira.
Awali,mikopo ya asilimia 10 ilikuwa ikitolewa kwa makundi mawili ya vijana na wanawake kwa masharti ya riba ya asilimia 10 kwa mwaka,lakini Mwaka 2017,serikali iliziagiza mamlaka za serikali za mitaa kuongeza kundi la walemavu ili kuweza kusaidia makundi hayo matatu kujikwamua kiuchumi.
Mwaka 2018, serikali ilitoa muongozo kuwa mikopo hiyo itolewe bila riba ili kuwapa fursa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu kwa ajili ya kuanzisha miradi kwa wingi ya kujikwamua kiuchumi kwani suala la riba limekuwa kikwazo kwa makundi mengi kuweza kukopa na kurejesha mikopo kwa wakati.