Diwani wa Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya akisoma taarifa ya Kata yake ya miezi mitatu ikiwemo mikopo kwa vikundi nane vya wanawake na vijana vilivyopata shilingi milioni 47, nyumba ya walimu shule ya msingi Ngage A imefika hatua ya jamvi na kutumia shilingi milioni 7, ujenzi unaendelea wa mfereji wa Malika Kijiji cha Loiborsoit B uliotengewa shilingi milioni 16.5 na mfereji wa Songoyo Ngage shilingi milioni 8.3 ila ubovu wa barabara zinazosafirisha mazao kwenda masoko nje ya Loiborsoit ni changamoto.
……………………….
Na Mwandishi wetu, Simanjiro
DIWANI wa Kata ya Loiborsoit Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, Siria Baraka Kiduya amesoma taarifa ya maendeleo na changamto zinazowakabili kwa mwezi Oktoba 2022 hadi Januari mwaka 2023.
Kiduya akisoma taarifa ya Kata hiyo kwenye kikao cha Baraza la Madiwani ametaja miradi iliyotekelezwa kwa muda wa miezi mitatu ni ujenzi wa nyumba ya walimu shule ya msingi Ngage A kwa gharama ya shilingi 7,000,000 na ipo hatu aya jamvi.
Ametaja miradi mingine ni mfereji wa Malila uliopo Loiborsoit B, uliogharimu shilingi 16,560,000 kazi inaendelea, shule ya msingi Songoyo imetengewa shilingi 10,000,000 na wananchi wamechangia mchanga na mawe.
Amesema mradi mwingine ni wa maji wa World Vision wa Ngage wa gharama ya shilingi 111,390,354 ujenzi umeanza awamu ya pili, baada ya uchimbaji wa mfereji kukamilika, pump house na tanki moja la kuhifadhi maji.
Ameeleza kuwa kwa upande wa vikundi vya Kata hiyo vilivyopata mikopo kwa mwaka 2021 hadi 2022 ni vikundi tisa kwa gharama ya shilingi 47,000,000.
“Vikundi hivyo ni Nyaru shilingi 5,000,000 Wanawake wapambanaji shilingi 5,000,000 na Enaboishu Vijana shilingi 6,000,000 vya kijiji cha Loiborsoit B,” amesema Diwani huyo.
Ametaja vikundi vingine ni Tujiinue vijana shilingi 7,000,000 Amani shilingi 7,000,000, Lang’ata shilingi 6,000,000 Elimika shilingi 6,000,000 na Vijana wazalendo shilingi 5,000,000 vya kijiji cha Ngage.
Kwa upande wa afya amesema kutokana na ongezeko la wakazi wa Kata ya Loiborsoit, wananchi wanaomba kusogezewa huduma za kituo cha afya ili kusogeza huduma karibu.
“Wananchi wamekuwa wakipata adha ya kwenda mbali nyakati nyingine hushindwa kupata huduma kutokana na ukosefu wa miundombinu rafiki katika kufikia vituo vya afya na hata kupoteza maisha,” amesema Kiduya.
Amesema kwa upande wa miundombinu daraja ni changamoto kwa wakazi wa kata hiyo kwa umuhimu wanaomba daraja litakalorahisisha huduma za kijamii na kuunganisha wananchi wa Simanjiro na Wilaya ya Same.
Ameeleza kuwa kwenye kilimo kuna changamoto ya ukosefu wa wakala wa mauzo ya mbolea ya ruzuku kwa mwaka 2022-2023 kwani wakulima wanapata tabu na uhitaji ni mkubwa kwani Kata ya Loiborsoit kilimo ni mwaka mzima.
“Kuna ubovu wa miundombinu ya skimu ya Malila na Ngage na ubovu wa barabara inayosafirisha mazao kwenda nje ya Kata ya Loiborsoit,” amesema Kiduya.
Amesema pia kwenye kata hiyo kuna upungufu wa maji mtoni na usumbufu wa mifugo mashambani kutokana na ukosefu wa malisho ya mifugo.
“Pia kuna kuongezeka kwa mbung’o katika kijiji cha Ngage, machinjio katika kijiji cha Ngage na kutengwa kwa maeneo ya malisho,” amesema Kiduya.