MKURUGENZI Bodi ya Maji,Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa fupi ya Utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo leo Februari 7,2023 jijini Dodoma.
MKURUGENZI Bodi ya Maji,Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,akifafanua jambo kwa waandishi wa habari (hawapo pichani) wakati akitoa taarifa fupi ya Utekelezaji wa majukumu ya bodi hiyo leo Februari 7,2023 jijini Dodoma.
MKURUGENZI wa Idara ya Habari Maelezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa,akizungumza mara baada ya Mkurugenzi Bodi ya Maji,Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,kutoa taarifa fupi ya Utekelezaji wa Majukumu ya bodi hiyo leo Februari 7,2023 jijini Dodoma.
………………………….
Na Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Bodi ya Maji,Bonde la Wami/Ruvu Mhandisi Elibariki Mmassy,amewataka wananchi kujiepusha na uchimbaji wa visima vya maji kiholela ili kulinda hazina ya maji iliyopo pamoja na usalama wa maji kwa watumiaji.
Mhandisi Mmassy ametoa wito huo leo Februari 7,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na wandishi wa habari kueleza utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo ambapo amewataka wananchi kutochimba visima kiholela bila kujua hali ya mfumo wa maji katika eneo husika.
”Uchimbaji wa visima bila vibali kuna sababisha uchafuzi wa maji chini ya ardhi na hatimaye kuleta madhara kwa afya kwa watumiaji hivyo tunawaomba wananchi wasichimbe visima hivyo kiholel”amesema Mhandisi Mmassy
Aidha Mhandisi Mmassy amesema kuwa bodi hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wananchi kufanya shughuli za kilimo maeneo ya jirani na vyanzo vya maji hali inayopelekea kuharibu vyanzo hivyo.
”Shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji kama vile kilimo, mifugo, uchenjuaji wa madini, uchepushaji wa maji mtoni, ukataji wa miti na uchomaji wa miti holela,vinasababisha uharibifu wa vyanzo vya maji nchini” amesema
Hata hivyo amesema kuwa wami/Ruvu ipo katika kampeni ya upandaji wa miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji ambalo ni jukumu lao kutekeleza agizo hilo lililotolewa na Mh. Makamu wa Rais Philip Isidory Mpango ambaye aliagiza kila Bonde kupanda miti milioni mbili.
”Waziri wa Maji Jumaa Hamidu Aweso alizindua rasmi kampeni katika Mkoa wa Morogoro Tarehe 03/01/2023 katika chanzo cha Mto Mbezi kinacho tumiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira (RUWASA).”amesema Mhandisi Mmassy
Amesema kuwa mpaka sasa Bodi imeanzisha kitalu chenye idadi ya miti 20,000 na kuendelea kuzalisha miti mingine itakayo kuwa inapandwa maeneo mbalimbali katika vyanzo kulingana na uhitaji.
”Tumefanikiwa kupanda miti elfu kumi na sita na mia sita (16,600) katika maeneo ya vidaka maji vya Ngerengere, Lukulunge, Bwawa la Mindu, hifadhi ya maji Makutupora, Mto Tegeta, Mpiji na Mto Kizinga. ”amesema
Aidha, amesema kuwa Bodi itaendelea na upandaji wa miti katika kipindi cha mwezi Machi hadi Mei, 2023 ili kutekeleza na kufikia lengo.
Ameongeza kuwa Bodi ya Maji kwa kushirikana na wadau mbalimbali ikiwemo ofisi ya Mkoa wa Morogoro imeandaa kampeni ya upandaji miti rafiki wa maji katika vyanzo vya maji inayo tarajiwa kufanyika Mwezi Februari 2023 katika eneo la Mindu Morogoro.
”Dhumuni ni kuendelea kutoa elimu kwa jamii na wadau mbalimbali juu ya umuhimu wa uhifadhi wa vyanzo vyetu vya maji hasa kwakupanda miti rafiki wa maji kwenye vyanzo vya maji.”amesema Mhandisi