MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 6,2023 jijini Dodoma kuhusu kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao kitafanyika kuanzia Februari 8 hadi 10, mwaka huu jijini Arusha.
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba,akifafanua maswali mbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo Februari 6,2023 jijini Dodoma kuhusu kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao kitafanyika kuanzia Februari 8 hadi 10, mwaka huu jijini Arusha.
…………………………………..
Na.Alex Sonna-DODOMA
MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA), Mhandisi Benedict Ndomba, amesema wadau 1000 wanatarajia kuhudhuria kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao ili kujadili mikakati mbalimbali ya kukuza serikali mtandao nchini .
Hayo ameyasema leo Februari 6,2023 jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kikao hicho kitafanyika kuanzia Februari 8 hadi 10, mwaka huu jijini Arusha na kitafunguliwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Jenista Mhagama.
Mhandisi Ndomba, amesema kuwa Mamlaka imejipanga kuweka mwelekeo wa serikali mtandao katika miaka ijayo kwa kuandaa na kutekeleza mikakati madhubuti ili serikali mtandao ifikie kuwa na sehemu moja ambayo huduma mtandao zote zitakuwa zinapatikana.
“Uwezo wa kutumia teknolojia mpya zinazoibuka, hasa zile za akili bandia, sarafu za kidijiti na teknolojia za kifedha, ili kuwezesha maboresho ya kiutendaji katika taasisi za umma na utoaji wa huduma kwa umma,”amesema Mhandisi Ndomba
Aidha amewataja wadau watakaoshiriki ni kutoka katika mashirika na taasisi za umma wakiwemo Maafisa Masuuli, Wajumbe wa Bodi, Wakuu wa Vitengo vya Tehama, Maafisa Tehama, Maafisa Rasilimali watu, Maafisa Mipango, Maafisa Mawasiliano, Wahasibu pamoja na Watumiaji wote wa Mifumo ya Tehama Serikalini.
“Kikao kazi cha tatu cha Serikali Mtandao kinaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Mifumo Jumuishi ya Tehama kwa utoaji huduma bora kwa umma’, lengo ni kuboresha utendaji kazi katika taasisi hizo pamoja na utoaji wa huduma bora kwa wananchi,”amesema
Hata hivyo ametaja baadhi ya mafanikio yatokanayo na e-GA ni kusimamia uziangatiaji wa sera, sheria na miongozo ya serikali mtandao kwa taasisi za umma.
“Kuwezesha usanifu na ujenzi wa mifumo ya serikali mtandao ya kitaasisi na ya kisekta ili kuboresha utoaji huduma kwa umma, kuboresha na kuongeza mawanda ya kusimamia uendeshaji wa miundombinu shirikishi ya serikali mtandao,”ameeleza