MAWAKALA wa Utalii wameanza kumiminika nchini ili kuangalia vivutio vya Utalii hapa nchini na kwenda kuvitangaza nchini mwao.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Prof. Eliamani Sedoyeka jana aliongoza mapokezi ya Mawakala hao kutoka katika masoko ya kimkakati katika nchi tofauti.
Nchi walizotoka Mawakala hao ni Marekani, Canada, Mexico, Ubelgiji na Brazil.
Akizungumza mara baada ya kuwapokea Mawakala hao, Prof. Sedoyeka amesema “Leo tumeanzisha Mega Trip ambayo kwa kawaida Wizara kupitia Bodi ya Utalii ( TTB) uandaa safari kama hizi ambazo uwaleta waongoza Utalii, Waandishi wa Habari na wadau wakuu wa utalii wa kimkakati ili waje Tanzania kuangalia maeneo yetu mbali mbali ya vivutio”.
Sedoyeka amesema watalii wanavyokuja nchini uletwa na makampuni ambayo tayari kama nchi imeshawajengea uwezo Mawakala wa nchi hizo juu ya vivutio vilivyopo nchini.
“Ziara hii inakuja baada ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuwa na mashirikino mazuri na kampuni ya Ndege ya Qatar na pia ni muendelezo wa matunda ya Royal Tour iliyoongozwa Mheshimiwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan. ” Amesema Sedoyeka
Amesema, Tanzania imeingia makubaliano ya kimkakati kuanzisha mahusiano ya kibiashara ili kuwatangazia duniani kuwa Tanzania kuna vivutio vya aina gani, mahusiano ya kimkakati ili kumtengenezea mtiririko wa wageni.
Amesema, kufunguka kwa masoko ya kimataifa yanasaidia kukua kwa uchumi wa nchi na kuongezeka kwa pato la taifa. Wafanyabiashara wanapata fedha.